SHARE

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk.Hamisi Kigwangala amezindua kamati ya kitaifa ya kuandaa Mwezi maalumu wa maadhimisho ya Urithi wa Taifa la Tanzania.

 Kamati hiyo inahusisha Wakuu wa Mikoa ambao pia ni wajumbe wateule wa Kamati ya kitaifa ya kuratibu shughuli za maandalizi ya Mwezi Maalum wa Maadhimisho ya urithi wa Tanzania.

 Akizungumza Dar es Salaam leo, wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, Dk.Kigwangala amesema anawapongeza  wajumbe wote wa Kamati ya Maadhimisho wa Mwezi wa Urithi wa Tanzania kwa kuteuliwa kwao kwa ajili ya shughuli hii muhimu katika kuhimiza urithi wa Tanzania kwa maendeleo ya sekta ya utalii katika Taifa letu.

Amesema sekta ya utalii imekuwa mhimili muhimu katika ukuaji wa uchumi  wa Tanzania ambapo kwa mwaka 2017 sekta ya  utalii imechangia dola za kimarekani Bilioni 2.1 takriban asilimia 25  ya  fedha za kigeni.

Amesema takwimu zinaonesha mwaka 2016 idadi ya watalii waliotembelea nchi yetu walifikia 1,284,279. Katika taarifa yake ya 6 ya maendeleo ya uchumi, inayoitwa “Unlocking the Potential of the Tourism Industry for Tanzanians” Benki ya Dunia inaonesha kuwa mapato ya utalii yatakua kila mwaka na kufikia Dola za Marekani 16 bilioni ifikapo 2025. 

“Hata hivyo, mpaka sasa sekta ya utalii Tanzania imekua ikijikita zaidi katika utalii wa wanyamapori ili kuvutia watalii ambapo takriban asilimia zaidi ya 80 ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Tanzania bara huja kuona wanyamapori.

“Nchi yetu imejaliwa kwa kuwa na rasilimali mbalimbali za urithi wa Taifa nje ya zile za wanyamapori. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaliwa kuwa na rasilimali za kipekee duniani zinazobainisha harakati za maendeleo ya binadamu kama vile chimbuko lake, teknolojia alizotumia.

”Na namna ambavyo binadamu amekuwa akitumia mazingira yake ili kumwezesha kuishi kwa zaidi ya miaka milioni tatu iliyopita. Mfano wa rasilimali hizo ni masalia ya Binadamu wa Kale (Zamadamu) walioishi Bonde la Olduvai zaidi ya miaka milioni 1.7 iliyopita na nyayo za Zamadamu aitwaye Australopithecus afarensis aliyeishi Laetol miaka milioni 3.6   iliyopita”amesema.

Pia miji ya kihistoria kama vile Bagamoyo na Kilwa, michoro ya miambani, Kondoa na mapango ya Amboni.Aidha Tanzania ikiwa na zaidi ya makabila 120 imejaliwa kuwa na anuaia za mila, desturi, vyakula, misemo, imani, mavazi, nyimbo, ngoma za aina mbali mbali na matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kuunganisha Watazania. 

Dk.Kigwangala amesema kutokana na kuona hayo yote wizara yake imeamua kuwepo na mwezi maalumu kwa ajili ya kusheherekea Urithi wa Taifa la Tanzania.

 Amesema Urithi huo wa Taifa ni miongoni mwa vivutio vya utalii kwa kuwa ni  vielelezo vya historia,  utamaduni na ustaarabu wa jamii katika hatua mbalimbali za maisha.

Ameongeza urithi huo huonesha na kuikumbusha jamii husika chimbuko la tabia, mila na desturi ambazo inazitumia katika nyanja za uchumi, siasa, teknolojia na elimu.

“Jamii yoyote ile inatambuliwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa kutokana na urithi wake. Kwa sababu hiyo, tuna kila sababu ya kuendeleza urithi huu tuliojaliwa na mwenyezi Mungu.

” Kwa kutambua umuhimu huo,kuuenzi, kuutangaza na kuutumia urithi wa Taifa la Tanzania kama kivutio cha utalii na kumbukumbu za Taifa, Wizara yangu imeona ni vema kukwepo na mwezi maalum wa kusherehekea Urithi wa Taifa la Tanzania (Tanzania National Heritage Month).Tumekubaliana mwezi huo utakuwa ukiadhimishwa kila ifikapo Septemba ya kila mwaka,”amesema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here