SHARE

Kocha wa Real Madrid Mfaransa Zinedine Zidane amesema hana presha na kazi yake kwani anajua hawezi kuwa kocha wa timu hiyo kwa miaka kumi hivyo utafika muda atafukuzwa.

Zidane amelazimika kuongelea jambo hilo baada ya kuwepo kwa tetesi nyingi kuwa huenda akafutwa kazi kutokana na mwenendo mbaya wa timu yake kwenye ligi kuu ya Hispania La Liga.

”Nimejitahidi kutoruhusu presha kutoka nje na ndani ya klabu kwasababu najua ipo siku nitaacha kufundisha hapa, siwezi kuwa hapa kwa miaka 10, najitahidi kutumia muda wangu kufanya kila kitu kwaajili ya klabu”, amesema Zidane kwenye mahojiano na kituo kimoja cha Runinga nchini Ufaransa ambako ameenda kwa mapumziko mafupi.

Zidane mwenye miaka 45 ameongeza kuwa, ”Kazi ya ukocha ukiwa unapata matokeo mazuri kila kitu kinakuwa shwari, lakini mambo yakiwa kama sasa ilivyo kwetu kila mtu atahoji uwezo wako, ndio mana najitahidi kuepuka kusikiliza wanasema nini”.

Nyota huyo wa zamani wa klabu hiyo aliteuliwa kama kocha mkuu mwaka 2016. Amefanikiwa kutwaa mataji zaidi ya Saba ikiwemo makombe mawili ya UEFA. Msimu huu timu yake haijaanza vizuri mbio za kutetea ubingwa wa La Liga ambapo hadi sasa inazidiwa alama 16 na vinara Barcelona.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here