SHARE

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) amewatunuku vyeti watoa huduma wa kujitolea wanaoshughulikia usimamizi wa mashauri ya watoto ili kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili katika Manispaa ya Mpanda wakati alipofanya ziara ya siku mbili ya kuamsha ari ya wananchi kushiriki shughuli za maendeleo mkoani Katavi.

Dkt Ndugulile amesema kuwa kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008) na Sheria ya Mtoto (2009), walezi, wazazi na jamii ina jukumu la msingi la  kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili katika ngazi ya familia, shuleni, mtaani na katika jamii zetu ikiwa ni pamoja na kutekeleza wajibu wa kupunguza mashauri ya watoto na kuwezesha watoto kupata huduma zao za msingi.

“Niwashukuru watoa huduma wanaojitolea kushughulikia usimamizi wa mashauri ya watoto kwa kwa kusaidia kuendeleza maslahi ya watoto kwa kuimarisha ulinzi na usalama dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wanaofanyiwa watoto katika jamii kwa kazi nzuri ya usaidizi na ulezi mnaoufanya” alisisitiza Mhe. Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi Bi. Agness William amesema jumla ya watoa huduma 105 walipatiwa mafunzo ya Usimamizi wa mashauri ya Watoto kwa ngazi ya jamii.

Aidha, Mkuu wa  Wilaya ya Mpanda Mhe. Lilian Matinga amesema kuwa Serikali itawapa ushirikiano wa karibu katika kupata majawabu ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakati wote wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao wa kusimamia mashauri ya watoto.

Naye Mwakilishi wa Shirika la JSI Bw. Chacha Mansori amesema kuwa Shirika lake litaendelea kuhamasisha watoa huduma wa kujitolea wanaoshughulikia usimamizi wa mashauri ya watoto ili kuimarisha ulinzi na usalama dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyojitokeza na kusaidia utoaji wa huduma kwa watoto walioathirika dhidi ya ukatili.

Mmoja wa watoa huduma wa kujitolea wanaoshughulikia usimamizi wa mashauri ya watoto ili kuimarisha mtandao wa ulinzi na usalama dhidi ya vitendo vya ukatili katika Manispaa ya Mpanda Bi.Joyce Joseph ameishukuru Serikali kwa kuwaona na kutambua umuhimu wao na kuwawezesha vifaa kwa ajili ya kufanya shughuli zao.

Sanjari na kupata mafunzo ya weledi wa usimamizi wa huduma ya mashauri ya watoto katika manispaa ya Mpanda, wahudumu hao wa kujitolea wamesaidiwa baiskeli 11 kwa ajili ya kufuatilia na kuwatembelea wahanga wa ukatili katika vitongoji na mitaa ya manispaa ya Mpanda.

Bi. Flora Cosmas kwa niaba ya watoto huduma hao ametoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) kwa kukubali kukutana nao, kuwatunuku vyeti vya utambuzi, na tuzo ya baiskeli kwa ajili ya kurahisisha kazi zao za kila siku.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here