SHARE

Na : HASSANI S. MNYONE

Ukubwa wa Tanzania unaendana na upatikanaji wa rasilimali na fursa nyingi za kibiashara ambazo zinaweza kusaidia kwenye uzalishaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Kwenye wilaya na mikoa mipya Tanzania zipo fursa nyingi ambazo waliotangulia wachache wanaendelea kuzifaidi na kukua. Ni vizuri vijana wa maeneo haya na maeneo mengine Tanzania tukafikiria zaidi kutoka tulipo na kwenda mbali kuibua na kuwekeza kwenye maeneo haya mapya. Fursa kadhaa ambazo nitazitaja hapa nimezishuhudia na kuzifanyia tafiti kwenye maeneo kadhaa ambayo nimefanikiwa kufika mwaka 2017, nimekuwa jicho lako kwenye maeneo ambayo hujafanikiwa kufika na hapa nakuletea fursa zinazopatikana kwenye mikoa kama Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi na Songea.

1: Usafiri na Usafirishaji

Ni biashara ambayo inahitaji mtaji mkubwa kidogo kwaajili ya kununua vyombo vya usafiri imara na vinavyoweza kushindana. Kwenye maeneo haya biashara ya kusafirisha abiria ni kubwa na inahitajika sana kwa watu kutoka maeneo yao kwenda mijini kwaajili ya shughuli za kibiashara na mahitaji mengine, mbali na kusafirisha abiria ipo nafasi ya kusafirisha mazao ya kilimo na usafirishaji wa vitendea kazi vya ujenzi kama vile mchanga, saruji, matofali na vingine.

2: Huduma za Chakula

Hii ni biashara ya kipekee ambayo mara nyingi haichagui eneo ili kuweza kufanya vizuri, kikubwa ni kuwa na mazingira safi ya kufanyia biashara na kupika chakula kizuri, kitamu chenye ubora. Zipo tayari biashara za chakula kwenye maeneo haya lakini bado hazjipata ushindani mkubwa wa watu wenye ubora na ubunifu kwenye upishi. Vijana waangalie fursa hii kwa jicho la kipekee.

3: Ujenzi wa Nyumba:

Kwenye miji mipya yote kuna ukuaji wa kasi sana kwenye sekta ya ujenzi na miundombinu ili kukidhi mahitaji ya makazi na mawasiliano kwa njia ya barabara pia. Ujenzi wa nyumba ni kwaajili ya wenyeji na wengine wageni ambao wanaweza kutumia nyumba kwa kukodisha. Hapa fursa zipo kwa kijana anayejenga anaweza kwenda kufanya kazi kwenye maeneo haya lakini kwa yule mwenye mtaji mzuri anaweza kujenga nyumba ambayo anaweza kupangisha na kupata fedha kwa muda mrefu.

4: Uuzaji wa bidhaa za ujenzi

Fursa ya ujenzi wa nyumba na miundombinu tofauti kwenye maeneo haya unaendana sanjari kabisa na uhitaji mkubwa wa bidhaa za ujenzi ambazo nyingi zinapatikana mbali sana na zile zilizopo karibu zimekuwa hazitoshelezi na wakati mwingine ni bei ya juu sana. Ukifanikiwa kufungua biashara hiyo maeneo haya uhakika kwa kufanya vizuri wa muda mrefu upo.

5: Uuzaji wa bidhaa za nyumbani (Jumla na rejareja)

Mahitaji ya vitu vya dukani ni makubwa sana kwenye maeneo haya kutokana na ukuaji wa kasi na kuchangamka kwa miji hii ambako kunakwenda na ongezeko la watu. Watu wanahitaji bidhaa nyingi na bora ziwe karibu nao na sio kuzifuata mbali wastani wa kutumia nauli ya Shilingi 6,000 mpaka 7,000 kwenda na kurudi, umbali wa KM60 mpaka KM70. Hii ni fursa kubwa sana kwasababu kando na kuhudumia mtu mmoja mmoja lakini nafasi ya kuhudumia biashara nyingine upo, biashara ambazo zitakuwa zinahitaji huduma na bidhaa zako ili nazo zijiendeshe.

6: Uwekezaji kwenye Kilimo

Sifa kubwa ya maeneo mapya ambayo na mimi binafsi nimefanikiwa Kutembelea ni kuwepo kwa radhi nzuri yenye rutuba yakutosha na ardhi hiyo inapatikana kwa bei nafuu sana ukilinganisha na maeneo mengine. Utakubaliana na mimi kuwa ukanda wa nyanda za juu kusini kuna utajiri mkubwa sana wa ardhi unayoweza kuzalishia matunda ya aina zote, mchele, Mahindi, viazi, mbogamboga, ngano, soya na mengine. Fursa hapa ni ardhi yenye rutuba na upatikanaji wa ardhi hiyo kwa gharama ndogo kabisa.

8: Uwekezaji kwenye Ufugaji

Wenyeji tayari wapo kwenye utaratibu wa ufugaji mzuri kabisa wa kimazoea ambao umewasaidia sana kwenye kupata mahitaji muhimu. Unaweza ukarukia fursa hii kwa kuwekeza kidogo kidogo kwenye ufugaji wa ng”ombe wa maziwa kwasababu utumiaji wa maziwa ni mkubwa kwa mtu mmoja na biashara za vyakula. Lakini pia fursa ipo kwenye ufugaji wa kuku wa nyama na mayai, pia maeneo ya kufanya shughuli hizi yapo kikubwa ni kufuata sheria na taratibu kwenye upatikanaji wa maeneo.

9: Shule za watoto wadogo

Kwa familia za wenyeji na zile zinazohamia kwenye maeneo haya mapya wanakutana na changamoto ya maeneo ambayo wanaweza kuwapeleka watoto wao wakashinda huko na kupata elimu kidogo. Hapa kinachohitajika sana ni majengo machache na mazingira safi yenye mvuto yana ruhusu motto kupenda kujifunza na walimu wazuri wachache. Ni gharama sana kama utahitaji kufanya mambo yote kwa wakati mmoja lakini ukianza kidogo kidogo unaweza kukua kwa haraka zaidi na gharama zisiwe kubwa sana.

10: Huduma za Nishati ya mafuta

Hii inaweza ikawa ngumu kidogo kwasababu ya ukubwa wa mtaji unaohitajika kuwekeza na kuendesha biashara hii lakini ni fursa adhimu sana kwa mwenye mtaji anaweza kuitumia hii na akafanya vizuri sana.  Uwepo wa pikipiki nyingi, magari ya taasisi tofauti tofauti, watu binafsi na mashine nyingine zinazotegemea nishati ya mafuta. Maeneo kama Igwachanya (Wilaya ya Wanging”ombe) na Makete kwenye mkoa wa Njombe, fursa hii ipo.

Huu ni uzoefu nilioupata kwenye maeneo mengi mapya, kutokea ngazi ya mkoa, wilaya mpaka vijijini. Vijana ndio tunategemewa zaidi kuwa na macho ya kuona fursa na roho za ujasirili kuanza kuzifanyia kazi fursa hizi adhimu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here