SHARE

Fahamu zangu zilipokuja kurudi nikajikuta nikiwa nimelala kitandani ndani ya kajumba cha udogo, chumba kilikuwa kidogo na chenye makolokolo mengi sana. Ilionekana hakuwa usiku ila kulikuwa na kagiza kutokana na mwanga kuingia kwa taabu ndani ya kachumba kale. Afya yangu haikuwa mbaya sana kama ilivyokuwa wakati nilipopoteza fahamu, kwani sikuwa na maumivu makali ambayo nilikwa nikiyahisi kabla, pia kile kikohozi kilichokuwa nami muda wote kilikuwa kimeniachia, nikajaribu kupapasa mgongoni kuona kama lile jeraha lilikuwepo nikakuta lipo, lakini lilikuwa dogo sana tofauti na lilivyokuwa limefikia.

Nilitumia dakika kadhaa kufikiria nini kilikuwa kimetokea na kunusuru maisha yangu, nikajiuliza pale palikuwa wapi, mwisho nikaamua kujiaminisha kuwa itakuwa ndugu zangu walifanikiwa kupata mganga wa kweli, na pale palikuwa kwa mganga. Nikaamka na kutoka ndani ya kachumba kale, na mwisho nje ya nyumaba ile ndogo, macho yangu yakapokelewa na pori kubwa, kajumba kale kalikuwa kamezungukwa na pori pande zote, hakukuwa na nyumba nyingine wala mtu ambaye nilimuona, lakini kwa mbali nilisikia sauti ya kama mti unakatwa na watu wakiongea, nikaamua kufuata sauti hizo. Nikiwa kwa mbali kabla sijafikia sauti zile zilipokuwa zinatokea niliweza kuona kulikuwa na watu wawili, mwanamke na mwanaume na walionekana kuwa wanafanya kazi fulani, nilipozidi kusogea zaidi nikagundua kuwa yule mwanamke alikuwa mke wangu na yule mwanaume alikuwa Mnaro, Mnaro alikuwa akifua magome ya mti mmoja mkubwa kwa kutumia panga huku mke wangu akiokota magome yaliyokuwa yanaanguka chini na kuweka kwenye ungo ambao ulikuwa pembeni ya mti ule. Sasa nikawa nimewafikia nao wakaniona, mke wangu akaacha alichokuwa anakifanya na kunijia kwa mwendo wa haraka na kunikumbatia kwa furaha, alionekana kufurahia sana kuona nikiwa nimezinduka, sikujua nilikuwa katika hali ile ya kupoteza fahamu kwa muda gani. Mnaro yeye alinipuuza na kuendelea na kazi yake kama vile hakuniona, nadhani bado alikuwa na hasira kutokana na mimi kutofanikiwa kuokoa maisha ya mpenzi wake Sauda na kumtoosha Muifufu. Tuliachiana kwanza na mke wangu nikamsogelea Mnaro na kumsalimia, akaitikia lakini kama mtu ambaye ana kinyongo na mimi, niliona aikuwa na haki ya kukasirika maana hata kama ni mimi ingeniuma mke wangu kufia Muifufu, hivyo nikaamua kumvumilia nikijua alihitaji muda kuamua kunisamehe. Basi nami nikaanza kushiriki ile kazi japo sikujua walikuwa wakifua magome yale kwaajili ya nini, wakati naanza mke wangu alijaribu kunizuia akidai hali yangu ya afya bado haikuwa nzuri lakini Mnaro akamtaka aniache nifanye kazi ile kwani hali yangu iliuhusu na nilikuwa nikpaswa kufanya mazoezi ili kuendelea kuimarisha afya yangu.

Tuliporudi nyumbani pale kwa Mnaro mke wangu akawasha moto wa kuni, akayaweka magome yale ndani ya sufuria yenye maji kisha akayabandika. Tulikaa tukiongea japo waongeaji sana walikuwa mimi na mke wangu, Mnaro alikuwa kimya akisikiliza zaidi na wakati mwingine kujifanya kama anatabasamu, ila hakuwa muongeaji.

Mke wangu akanielezea kuwa baada ya kupoteza fahamu pale kwenye kikao walijaribu kunipeleka hospital na kwawaganga bila mafanikio, maombi pia ya dini zote hayakuzaa matunda. Mwisho wakaamua kuniacha nyumbani tu kungojea mauti yangu, “kwakweli tulikata tamaa, tulijua tumeshakupoteza tayari” alisema mke wangu na kufikia hapa akashindwa kuzuia kilio, nami nikafanya kazi ya kumbembeleza, ambayo ilifanikiwa kisha akaendelea kunithimulia kuwa nikiwa nina wiki ya pili toka niwe katika hali ile ya kutokuwa na fahamu, Mnaro akawaendea na kuwaambia kuwa alikuwa na uwezo ya kunisaidia lakini alitaka kuondoka na mimi na ataenda kunitibia ambako angejua yeye lakini ningerudi nikiwa mzima, ndugu zangu wakamkatali naye akaondoka, lakini usiku wa siku hiyo akaja katika chumba ambacho nilikuwemo, na mke wangu alikuwemo akilala na mimi, akamshawishi mke wangu kumruhusu anichukue akanitibu, “kwakweli hata mimi nilikuwa naogopa sana kumkabidhi kuondoka na wewe, maana baada ya kujitambulisha nilijua yeye ni nani maana ulikuwa umenielezea uwezo wake mara kadhaa, sikujua kama alikuwa na nia ya kukusaidia au kukulipizia kisasi maana najua ana hasira na wewe” alelezea mke wangu, lakini baadae ikambidi kujaribu kwakuwa hakukuwa na namna nyingine ya mimi kupona, pia alikuwa anaujua uwezo wake, na alijua fika kuwa kama angeamua kufanya maamuzi ya kunichukua hakuna ambaye angeweza kumzuia, “hivyo niliweza kufanya ni kumsihi tu na mimi nije, nashukuru akanikubalia” . Kutoka kwenye maelezo haya ya mke wangu, nikajikuta nimegundua kuwa nilikuwa katika hali ile ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu maana ujio wa Mnaro tu ulitokea wiki ya pili baada ya kuwa katika hali ile, “inamaana nimekuwa katika kutojifahamu kwa muda gani?” niliuliza na mke wangu akaniambia nilikaa katika hali ile kwa mwezi mmoja na siku nne. Nilishangaa sana, kumbe nilikuwa katika hali ya nusu ufu kwa muda wote huo, mimi nilona ilikuwa ni kama jana tu.

Baadae baada ya giza kuwa limeingia Mnaro akamuomba mke wangu amuachie nafasi tuongee kidogo, jambo ambalo alitii. “sina chuki yoyote niliyonayo juu yako, hasira zangu zote zipo kwa Magigi, yeye ndiye aliyenitenganisha muda wote huo na Sauda, na niyeye aliyeuhukua uhai wake” alianzisha mzungumzo Mnaro, nikashukuru sana kusikia kuwa hakuwa katika ugomvi na mimi maana balaa lake nalijua, sikutaka awe adui yangu hata kidogo. “ndani ya muda mfupi tutapaswa kufanya safari ya kwenda Muifufu, inabidi tujiandae” aliongezea Mnaro na kuishtua nafsi yangu, mimi nilidhani kwakuwa afya yangu imerudi kuwa nzima basi sikuwa na haja tena ya kukifuata kifo Muifufu. “lakini mimi sina tena haja ya kwenda Muifufu, maana nimepona tayari” nilimjibu Mnaro ambaye aliniangalia kwa macho makali sana. “unadhani umepoana wewe? Wewe dawa yako ni kulipa ahadi uliyowekeana na jamii ya watu wa milima Kalingisi, ugojwa uliokupata unasehemu tatu,sehemu ya kwanza ndio hii ambayo tumefanikiwa kuitibu, sehemu ya pili mwili wako wate huo utavuka ngozi, ndo maana tunaandaa dawa ile, sehemu ya tatu ni kifo, hakuna ambaye anaweza kuzui isipokuwa kifo cha Magugi, sote tunataka jambo moja, lazima tushirikiane ili kulifanikisha” alisema Mnaro, maneno yake yakanitisha sana. “sasa kama niko tayari kwenda Muifufu na kumuua Magugi, kuna haja gani ya kuniandalia dawa,maana hiyo sehemu ya tatu ya ugonjwa huo haitonikuta. “hili eneo langu nimelizindika sana, halionekani kwa macho ya kawaida wala ya mchawi, hata ubaya wa Muifufu na mlima Kalingisi hauwezi kuingia kwenye himaya hii, ndio maana nimeweza kukutibia huku na umepona, kwenye dunia ya kawaida wewe ungekuwa mfu sasahivi” aliweka kituo kidogo kisha akaendelea. “kama ungeweza kubaki kwenye eneo hili tu, ugonjwa wako ungepona kabisa lakini maandalizi ya safari hii yatatutaka kwenda safari ya mbali ambapo hutokuwa na kinga yoyote, ndo maana tunaandaa dawa ile ambayo itakuwa ikipunguza makali ya ugonjwa, nasi tutapaswa kumaliza haraka kilichotupeleka huko kabla nguvu ya dawa haijazidiwa na ugon jwa” alielezea vizuri Mnaro, nilichanganyikiwa kuona jambo hili lilikuwa bado bichi namna ile, mimi nilidhani hatimaye sasa nilikuwa naelekea kupata amani baada ya afya yangu kurudi. “hiyo safari ni yakwenda wapi na kufanya nini?” niliuliza. “ni safari ya kwenda kwenye ufalme wa uchawi kutafuta nguvu ambayo itamuondosha Magugi na utawala wake kufumba na kufumbua tu” alielezea Mnaro. “Na huko kwenye ufalme wa uchawi ni wapi?” niliuliza kwa shauku baada ya kuona kuna matumaini kwenye safari hiyo. “ni ujinini, chini ya bahari” alijibu Mnaro.

Usikose sehemu ya 55


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here