SHARE

Maneno yale yalinifanya kumuona Mnaro ni kiumbe wa ajabu sana, anawezaje kuzungumzia habari za kwenda kwa majini kanakwamba anaongelea safari ya kwenda sokoni?, nikabaki nimepigwa na bumbuwazi, sikujua hata niseme nini. “uchawi ni elimu ya majini, sisi tuliabahatika kupata sehemu ndogo sana ya elimu hii na ndio tunaiumia kufanya yote tunayofanya, hebu fikiria huko ujinini ambako ndiko kwenye elimu yote wana uwezo kiasi gani?” aliendelea kunielezea Mnaro ambaye alionekana amedhamiria kweli kwenda ujinini na hakuwa na uoga hata kidogo. Nilimuona Mnaro kama mtu ambaye alikuwa amakata tamaa ya kuishi, hakuwa na lolote lililo zuri kwenye maisha yake, mafaniko pekee ambayo alikuwa anatamani kuyafikia ilikuwa kutoa uhai wa baba yake, mzee Magugi, na hakujali kama angepatwa na umauti katika kulitekeleza hilo, hakuwa na sababu ya kuishi. “kesho utapumzika ili afya yako ijijenge, kama mambo yakienda vizuri, keshokutwa tutaianza safari ya ujinini” alinieleza Mnaro na kikao kile kikaishia pale, niakaingia ndani na kujumuika na mke wangu ambaye alikuwa akinisubiria kwenye kale kachumba ambamo nilijikuta wakati nazinduka. Tuliongea mengi na mke wangu ambaye alikuwa na furaha zote akiamini kwamba matatizo yalikuwa yameisha na sasa tulikuwa tunenda kuyaanza upya maisha yetu,nikaamua kutomjuza chochote ili kutoharibu furaha yake, japo kwa wakati ule tu.

Kesho yake ilikuwa ni siku ambayo kwa kiasi kikubwa tulishinda mimi na mke wangu tukiwa pekeyetu maana Mnaro alikuwa na mizunguko mingi ambayo nilihisi ilihusiana na kujiandaa kwa safari ya kesho yake.

Mida ya jioni nikiwa nimepumzika na mke wangu, Mnaro alikuwa bado hajarudi, nikaamua kumuelezea mke wangu juu mambo yalivyo, nikamuelezea kuhusu safari ya kesho yake kuelekea ujinini na safari ya Muifufu mara baada ya kutoka ujinini. Mke wangu alisikittishwa sana lakini hakuweza kupinga kwani alikwisaona jinsi ilivyokuwa hatari kulipuuza lile jambo, maana ilibaki kidogo tu linitoe uhai. “hakuna namna, ni lazima kwenda ila tutakwenda pamoja” alisema mke wangu macho yake yakionekana kukimaanisha anachokisema. “hapana hii safari wewe huwezi kwenda ni hatari sana, kwanza mimba yako imekuwa sana, hutakiwi kukutana na misukosuko” nilijaribu kushuri lakini hakunielewa. “wewe uliniahidi kuwa hatuachani tena, siku zote tutakuwa pamoja, sisi ni familia na lazima tuwe pamoja kwenye shida na raha, hata huyu mtoto anataka kuwa nasisi pamoja, kama ni kufa tukafe wote” mke wangu hakuonekana kama angeweza kunielewa, nikona yeye alikuwa tatizo dogo san kulinganisha na matatizo ambayo yalikuwa mbele yetu hivyo nikaamua kumuacha aamini anachokiamini, “wakati utakapofika atabaki tu” niliwaza.

Jioni Mnaro akarudi, akaniita tukaanza kujadili juu ya safari yetu “ kwenye safari hii tunautegemea msaada wa jini ambaye atatufuata hapa alfajiri, atatupeleka mpaka ambapo hatuwezi kupotea kisha tutamalizia wenyewe”. Alinielezea Mnaro. Akanieleza kuw a jini huyo alikuwa mkazi wa huko ambako tunataka kwenda ila kuna kosa ambalo alifanya huko, hivyo akafukuzwa na kutakiwa kutorudi. “wewe unamuaminije kama atatusaidia, tusije tukaenda kujikuta tunaangukia matatizoni” nilionesha wasiwasi wangu. “jini huyu ninamdai, hii ndiyo njia yake pekee ya kulipa deni lake, hawezi kutuuza” alisema Mnaro. “duhh! Kwahiyo wewe unafanya mpaka niashara na majini?” niliuliza kwa mshangao. “majini ni viumbe tu ambao wameumbwa na Mungu kama mimi na wewe lakini cha ajabu kuna wanadamu wanaogopa majini kuliko Mungu mwenyewe” alielezea Mnaro. Nikaamua kuhama kwenye ile mada na kumuelezea juu ya mke wangu kung’ang’ania kuwemo kwenye ile safari na jinsi ambavyo sikutaka kabisa aende. “huyo sio tatizo, tutamudisha nyumbani usiku akilala na hawezi kutupata tena”.


1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here