SHARE

Alfajiri Mnaro akaniamsha na kunitaka kuwa tayari kwa kuondoka, pale kitandani mke wangu hakuwepo japo nililala nae. Nikajua bila shaka atakuwa amerudishwa nyumbani tayari. Tukatoka nje na kungojea, mara akaja binti mrembo sana akiwa juu ya farasi, farasi huyo alikuwa wa ajabu kidogo, alikuwa ni mweupe sana mpaka macho yanaumia kumungalia, pia alikuwa mkubwa sana na mwenye miguu sita baadala ya minne. Binti yule akatutaka sote kupanda kwenye farasi yule ambaye ukubwa wake ulitutosha sote vizuri tu, kisha safari ikaanza.

Farasi yule alienda mwendo wa kukimbia kama farasi wengine, lakini tulipotoka kwenye eneo la pori akaenda akipaa juu ya kuongeza kasi, kasi ikwa kubwa mpaka upepo ukawa unanitoa machozi. Ndani ya dakika kama 20 hivi niliona tumefika eneo la baharini, farasi yule akendelea kwenda kwa mwendo ulelule wa kupaa juu ya maji yale mpaka sehemu ambapo tulikuta maji ya bahari yakiwa kama yanachemka na kufanya duara kubwa ambapo katikati yake kuikuwa na uwazi, farasi yule akatua kwenye uwazi ule, tukadumbukia kwenye shimo refu sana ambalo kuta zake zilikuwa maji ya bahari. Shimo lile lilikuwa refu sana, ilimchukua farasi yule dakika kama saba mpaka kufik chini ambapo tulikutana na ardhi ya kawaida tu, farasi yule akaendelea kukimbia juu ya ardhi ile, mimi nikajaribu kutizama juu kuona kama nitayaona maji ya bahari lakini nikaona kulikuwa na anga la kawaida tu. Tulienda mpaka tukafika sehemu ambapo kulikuwa na lango kubwa la kuinglilia kwenye mji ambao ulionekana mbele yetu, farasi yule akasimama na binti aliyekuwa dereva wetu akatutaka kushuka, “mimi siruhusiwi kwenda zaidi ya hapa, hata ninyi mkionekna mmekuja na mimi hamtosaidiwa, endeleeni narudia hapa” alisema na farasi yule akaondoka kwa mwendo wa kasi. Kulikuwa kumeanza kupambazuka, tukaingia kwenye geti lile, tukawa tunatembea huku tukishangaa uzuri wa majumba yaliyokuwemo kwenye mji ule, ulikuwa na mji mdogo tu lakini kulikuwa na nyumba za kifahari sana na zilipangiliwa vizuri na kuufanya mji ule kuwa mji wa kupendeza sana

“ni nyumba hii” alisema Mnaro akionesha jumba moja kubwa sana, tukaenda na kubisha hodi, tukapokelewa na kijana ambaye alionekana kama alikuwa mfanya kazi katika jumba lile. “tunahitaji kuonana na mwenye nyumba hii” alisema Mnaro na kijana yule akatukaribisha ndani, akatupeleka kwenye eneo ambalo kulikuwa na ukumbi mkubwa wenye viti vingi sana mbele yake kukiwa na kiti kimoja cha heshima. Baada ya muda mfupi kijana yule akarudi akiwa ameongozana na kijana mwingine ambaye alikwenda na kukalia kile kiti kikubwa kilichokuwa mbele ya viti tulivyokalia. “baada ya kukaa kukatokea kitambaa kikubwa cheupe katikati yetu sisi na yeye, kitambaa hiki kilifanana na vitambaa vinvyotumika kuoneshea sinema, kwenye kitambaa kile yalianza kuonekana matukio yetu tuliyopitia mpaka kufika pale, kisha kikawa kinaonesha matukio ya nyuma, mpaka matukio ya kutoroka Muifufu yakaonekana, pia matukio mengine ya Mnaro ambayo sikuyajua yakaonekana. “Mlielekezwa kuja kuonana na baba yangu, ila kwa bahati mbaya ni marehemu kwa sasa, shida yenu inaweza kutatuliwa na ndugu yangu ambaye ndiye aliyerithi uchawai, mimi nilichagua kurithi utajiri” alisema kijana yule. “ndugu yangu huyo sikuhizi hakai hapa, mnaweza kupelekwa ambapo anakaa, ila nauona muishilio mbaya wa mmoja wenu” alisema kijana yule mwenye asili kama ya Kiarabu.

Usikose sehemu ya 57


3 COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here