SHARE

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul  Makonda amesimamisha shughuli zote za usikilizwaji wa kesi katika mabaraza ya  kata katika mkoa wa Dar es salaam, na kuzihamishia kwa makatibu tarafa na kuagiza kesi zote zilizopo katika mabaraza ya kata zihamishiwe na  kusikilizwa kwa makatibu wa tarafa mara moja.

Makonda ametoa agizo hilo jijini hapa wakati akipokea taarifa ya ripoti za malalamiko yaliyotolewa ambapo jumla ya wananchi 6552 walijitokeza na kusikilizwa na wanasheria 409 walikaa na kuyachambua kwa kina malalamiko ya wananchi hao na kutoa mrejesho wa baadhi ya malalamiko hayo na kumkabidhi.

Pia Makonda amesema shughuli za mabaraza ya kata zitarudi mara baada ya kupatikana kwa  wanasheria wanaojua masuala ya ardhi na kuagiza kuanzia jumatatu makatibu tarafa wote kupita katika mabaraza ya kata na kuzichukua kesi zote zilizopo sasa na kuzihamishia kwao na kupiga marufuku kwa madalali uchwara wanaouza mali za wananchi wanyonge wasiokuwa na hatia wala ushahidi na bila ya kufuata utaratibu kwa kisingizio cha kufuata amri ya mahakama.

“Naagiza siku ya jumanne saa nne madalali wote mnaotekeleza shughuli za Benki mfike ofisini kwangu ili tujiridhishe na wataalamu wangu kama kweli mnafaa kufanya hiyo kazi kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo, maana wengine mnafanya minada na kuuza mali za watu bila  kufuata utaratibu na kuwaumiza wananchi wanyonge” alisema Mhe. Makonda.

Aidha Makonda amewataka Wakurugenzi mbalimbali na wakuu wa idara kujitathimini kama wanafaa kuwepo  katika nafasi zao, na kuomba kuanzia jumatatu kupitia  wasifu (CV) za wakuu wa idara wote ili kupima na kuangalia utendaji wao wa kazi kama unaenda na nafasi zao walizokuwa nazo kwenye idara zao.

Kadhalika Makonda amesema kuwa kazi ya usikilizwaji wa malalamiko ya wananchi ataendelea nayo kuanzia mwaka huu hatoiacha na kusema ataanza kutembelea ofisi za kata kwa kushtukiza ili kuangalia mienendo ya kazi inayofanyika katika  ofisi hizo na endapo atabaini kuwepo kwa uzembe kwa watendaji hao hatosita kuwatimua mara moja.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here