SHARE

RELI ya Kisasa (SGR) inayojengwa hapa nchini imeelezwa kuwa ni reli bora kuliko zote Afrika. Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), ilianza awamu ya kwanza ya ujenzi Mei, 2017 na inajengwa na Kampuni ya Kituruki ya Yapi Merkezi kwa ubia na Kampuni ya Mota-Engil Africa ya Ureno.

Awamu hiyo ya kwanza ya ujenzi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ina urefu wa Kilomita 205 zikiwemo Kilomita 95 za njia za kupishania treni na kufanya reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kuwa na urefu wa Kilomita 300. Akizungumza na gazeti la Habari Leo, Meneja wa Mradi huo kutoka Rahco, Maizo Mgedzi alisema ubora wa reli ya kisasa inayojengwa Tanzania uko juu ikilinganishwa na ubora wa reli zilizojengwa kwenye baadhi ya nchi Barani Afrika.

Mgedzi, alizitaja baadhi ya nchi Barani Afrika ambazo zimejenga reli ya SGR kuwa ni pamoja na Ethiopia, Afrika Kusini, Kenya na Morocco. Alisema, reli zilizojengwa kwenye nchi hizo zina uwezo wa kupitisha treni zenye uwezo wa mwendokasi wa kilomita 120 tu kwa saa tofauti na reli inayojengwa nchini ya kupitisha treni za uwezo wa mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa.

“Lakini pia reli tunayoijenga itatumia treni za umeme tofauti na nchi nyingine nyingi ambazo treni zao zinatumia mafuta ya dizeli. Ethiopia wanajenga reli ya kutumia umeme na kipande kidogo cha reli ya abiria Johannesburg, Afrika Kusini nacho kinatumia umeme,” alisema. “Pia sisi tunajenga reli yenye uwezo wa kupishanisha treni zenye urefu wa kilomita mbili tofauti na nchi nyingine ambazo treni zao hazizidi kilomita moja; Viwango vya ubora wa reli tunayojenga Tanzania viko juu kuliko nchi nyingine,”alieleza Meneja wa Mradi, Mgedzi.

MATALUMA NA UPANA WA RELI Kwa kuzingatia ubora na uimara wa reli hiyo, serikali imeamua kujenga reli hiyo kwa kutumia mataluma ya zege na si ya chuma kama kwenye reli ya zamani ambayo inatumika mpaka sasa. Imeelezwa kuwa, reli inayojengwa kwa mataluma ya chuma ina uwezo mdogo zaidi ikilinganishwa na reli inayojengwa kwa mataluma ya zege.

Akifafanua faida ya kutumia mataluma ya zege kwenye ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea, Mgedzi alisema, mataluma ya zegeyataiwezesha reli inayojengwa kubeba mzigo wenye uzito mkubwa zaidi wa hadi tani 35 kwa ekseli tofauti na reli iliyopo sasa iliyojengwa kwa mataluma ya chuma ambayo haiwezi kuchukua mzigo mzito zaidi unaozidi tani 14 kwa ekseli.

Mgedzi alisema, mataluma ya zege yana uwezo wa kuhimili mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa kwa treni ya abiria na mwendokasi wa kilomita 120 kwa saa kwa treni za mizigo tofauti na treni ya sasa inayotumia mataluma ya chuma na mwendokasi wa kilomita 70 kwa saa. Kuhusu upana wa reli hiyo ya kisasa, mtaalamu huyo alisema itakuwa na upana wa milimita 1,435 ambao ni sawa na upana wa mita 1.435 tofauti na reli ya sasa yenye upana wa milimita 1,000 ambao ni sawa na upana wa mita moja.

“Upana mkubwa wa reli tunayoijenga sasa utaiwezesha treni inayotembea juu ya reli kuwa imara, kwenda kwa kasi na kuwa salama zaidi. Kwa hiyo reli tunayojenga ina upana wa milimita 435 zaidi ya reli inayotumika sasa.” “Na tunaposema ‘gauge’ maana yake ni upana wa reli.

Reli ina miguu miwili, yaani kulia na kushoto ambayo imeshikwa na mataluma, kwa hiyo upana kati ya reli moja na nyingine unaitwa ‘gauge,’” alifafanua Meneja Mgedzi. UWEZO WA KUBEBA MIZIGO NA ABIRIA Kwa kuzingatia viwango vya ubora, reli inayojengwa nchini, itakuwa na uwezo wa kupitisha mzigo wa tani kati ya milioni 17 hadi 25 kwa mwaka ikilinganishwa na reli ya sasa inayopitisha tani milioni tano kwa mwaka.

Kuhusu abiria, Mgedzi alisema, kutokana na urefu wa njia za kupishanisha treni, reli hiyo itaweza kusafirisha kiwango kikubwa cha abiria lakini kwa kuanzia itakuwa ikisafirisha abiria wasiopungua milioni 1.2 kwa mwaka. IDADI YA SAFARI DAR-MORO Kwa kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya usafiri, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kuwepo kwa treni tatu za abiria kama hatua ya mwanzo zitakazokuwa zikienda na kurudi Dar es Salaam na Morogoro kila siku.

Kwa mujibu wa Mgedzi, treni moja ya abiria inaweza kufanya safari zaidi ya 3 au 4 kwa siku kati ya Dar es Salaam na Morogoro, na hivyo kwa siku kunaweza kuwa na safari kati ya tisa hadi kumi na mbili, lakini idadi ya safari itaongezeka kulingana na abiria walivyo wengi. “Unapoanza na kitu kipya, una hatua ya awali ya kuvutia wateja na ili wateja waweze kuvutika unahitaji kutoa huduma ya uhakika, usafiri wa kasi na pasipo kupoteza muda kwa kusimama simama njiani, mambo hayo yatavutia tu wateja,” alieleza Meneja Mradi, Mgedzi.

IDADI YA STESHENI Reli hiyo ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ina stesheni sita, Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro. UHAI WA RELI Imeelezwa kuwa, uhai wa reli baada ya kukamilika na kabla ya kuanza kufanyiwa ukarabati wowote mkubwa, unategemea mifumo yake ilivyo kama madaraja, vyuma vya reli, mifumo ya umeme, pamoja na mifumo ya ishara na mawasiliano.

Akielezea uhai wa reli hiyo ya kisasa, Mgedzi alisema, madaraja ya reli hiyo yana uwezo wa kudumu kwa miaka 100, wakati reli yenyewe ambacho ni chuma kinachokanyagwa na kusuguliwa na tairi la chuma la treni, lina uwezo wa kudumu kwa miaka 40 kabla ya ukarabati. Kuhusu mifumo ya umeme na mawasiliano, alisema inategemea na aina ya mtambo na nyaya zitakazotumika, hivyo reli hiyo ya SGR alisema usanifu wa vitu hivyo bado unaendelea na taarifa za uhai wake zitatolewa baadaye.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here