SHARE

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesimamisha shughuli zote za mabaraza ya ardhi ya kata katika mkoa huo kwa kuwa yameonekana hayana uwezo wa kusikiliza kesi.

Wakati akitoa uamuzi huo, Mkuu wa Idara ya Ardhi Ilala, Paul Mbembela amepoteza fahamu na kukimbizwa hospitali baada ya kutangazwa kuwa apangiwe kazi nyingine kwa kutomudu majukumu hayo.

Aidha, amewataka wakurugenzi wa Manispaa za Ubungo na Ilala kuwapangia kazi nyingine wakuu wa ardhi wa manispaa hizo pamoja na Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Ustawi wa Jamii Ilala kwa kuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao katika idara zao.

Mbali ya hao, amemtaka Mkuu wa Idara ya Ardhi ya Mkoa ajipange na endapo atashindwa kutekeleza majukumu yake aandike barua ya kuacha kazi. Pia amewaagiza wakurugenzi wa manispaa zote za mkoa kupitia wasifu wa wakuu wao wa idara kwa kuwa kuna wengine hawana sifa ya kazi wanazozifanya. Makonda alitoa maagizo hayo kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jana wakati wa mkutano wa marejesho ya malalamiko ya wananchi zaidi ya 6,000 wa mkoa huo waliopatiwa msaada wa kisheria kwa siku tano bure.

Akizungumzia suala la mabaraza ya ardhi ya kata, Makonda alisema mabaraza mengi yamekuwa yakilaumiwa kushindwa kutenda haki kwa wananchi wakati wanapopeleka mashauri yao katika mabaraza hayo. “Kuanzia leo Februari 10 nasimamisha kazi zote za mabaraza ya ardhi ya kata katika mkoa wangu na kesi zote zilizopo katika mabaraza yao ziwasilishwe kwa makatibu tarafa na kuanzia Jumatatu nataka makatibu tarafa wapite kwenye mahakama hizo kuchukua kesi pamoja na hukumu zilizopo katika mabaraza hayo,” alisema.

Hatua ya wakuu wa idara waliosimamishwa imekuja baada ya kutakiwa kutaja idadi ya kesi za ardhi walizozipokea katika idara zao kutokana na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa hazifanyi kazi ipasavyo. Katika majibu yake, Mkuu wa Idara ya Ardhi Wilaya ya Ubungo, Khamis Songwe alisema wilaya hiyo haina kesi yoyote ya ardhi, hali mkuu wa mkoa ana takwimu ya kesi zilizopo.

Naye Mkuu wa Idara ya Ardhi Ilala, Paul Mbembela alitaja takwimu ambazo siyo sahihi na baada ya kauli ya Makonda kutaka apangiwe kazi nyingine, ghafla alipoteza fahamu na kukimbizwa hospitali. “Wakurugenzi naomba kuanzia leo watu hawa wapangiwe kazi nyingine hatuwezi kuwa na mtu ambaye hana uhakika na kitu anachokifanya hao ndio wanaharibu serikali ya Rais John Magufuli,” alisema Makonda.

Makonda alimkabidhi Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni majina ya watu wanaodaiwa kuhusika na udalali wa nyumba bila kufuata utaratibu, watendaji wa benki wanaofanya kazi zao bila kufuata utaratibu, watu wanaoghushi kadi za magari pamoja na watu wanaoghushi nyaraka na kuuza nyumba na maeneo ya watu na kuagiza watu hao waanze kukamatwa leo na Jumatatu wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewataka madalali wote wanaohusika kuuza nyumba kwa amri za benki pamoja na mahakama wafike katika ofisi yake keshokutwa wakiwa na nyaraka zao za usajili ili ajiridhishe na kuwafahamu. Makonda pia amewataka wananchi wote waliosikilizwa wafike katika ofisi yake Februari 19, kwa ajili ya kuwapatia mawakili ambao watasimamia kesi zao hadi wapate haki yao bila gharama yoyote.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here