SHARE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imebaini kwamba maeneo ya bahari kuu, bandari, vituo vya mabasi na viwanja vya ndege yanayotumika sana katika kupitisha dawa za kulevya.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema wafanyabiashara, wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya wameendelea kukamatwa, lengo ni kuhakikisha biashara hiyo inamalizika nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13, 2018) wakati akikabidhi gari kwa Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Siyanga  kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Amesema mbali na kukamata meli, pia Serikali imewakamata wasambazaji pamoja na kundi kubwa la wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya sambamba na watumiaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na kizazi chenye uwezo wa kuzalisha mali.

Waziri Mkuu amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulenya, ambapo hivi karibuni imekamata meli nyingi, moja ilikiwa inatokea pwani ya Msumbiji na ilikamatiwa maeneo ya Mtwara ikiwa na dawa nyingi za kulevya.

“Niwakati wa Serikali kuendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na leo hii tunawakabidhi gari hili jipya kabisa ili iweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo.”

Pia Waziri Mkuu amewataka Watanzania waachane na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na  kazi ya kusambaza, kuzalisha na kutumia na watakaokamatwa wakijihusisha nayo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema kwa sasa Serikali inajenga maabara ambayo itatumiwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa wanazozikamata.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here