SHARE

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimejitabiria ushindi wa asilimia 70 katika uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni unaotarajiwa kufanyika Februari 17, mwaka huu.

Meneja wa Kampeni za jimbo hilo na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema jana kuwa tathmini ambayo chama chake kimefanya katika kampeni zinazoendelea, uhakika wa Chadema kushinda ni mkubwa.

Alisema wanachopigania kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo ni kuhakikisha wasimamizi wa uchaguzi huo wanatenda haki kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi.

“Tunapigania haki itendeke kwa kuhakikisha Chadema tunatangazwa washindi baada ya wananchi kupiga kura na ndio maana tunapambana kuhakikisha hizi kasoro zinazoonekana zinatatuliwa ili uchaguzi ufanyike kwa uhuru na haki,” alisema Kubenea na kuongeza:

“Hatutakubali ‘abadani’ baadhi ya watu wachache wakatumika au kutumia nafasi zao vibaya kupindisha haki, tuna uhakika wa kushinda kwa sababu, tumepita kila nyumba jimbo zima, tunawajua watu wetu na tumewaandika katika daftari letu wapigakura wetu ambao tunajua ni wa uhakika na hawadanganyiki.”

Mkurugenzi wa Operesheni na uchaguzi wa Chadema, Benson Kigaila, alisema zipo kasoro ambazo zimeanza kuonekana za kuharibu uchaguzi huo ikiwamo kushindwa kuwapatia kwa wakati fomu za uapisho mawakala wa uchaguzi huo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here