SHARE

Simba imecheza na Gendarmarie mechi ya awali ya Kombe la Shirikisho na kushinda mabao 4-0, lakini katika kipindi chote cha mchezo, yapo mambo matano muhimu unatakiwa kuyajua.

Rais Mwinyi awa kivutio

Awali, haikufahamika wazi kwamba Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ni shabiki wa Simba lakini katika mchezo wa Simba na Gendarmarie ni kama ilijidhihirisha wazi kwamba yuko upande wa huo wa Msimbazi.

Na hii ni baada ya kualikwa kuwa mgeni rasmi wa mchezo baada ya kuwa kimpya kwa kipindi kirefu na ndani ya suti yake, alikuwa amevalia tisheti nyeupe yenye ufito mwekundu inayofanana kabisa na zile jezi za Simba.

Kichuya kuvaa hereni

Haijawahi kutokea au kama iliwahi kuonekana ni mara chache kwani mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya aliingia kucheza mchezo huo akiwa amevalia urembo masikioni.

Kichuya alivaa urembo huo unaofanana kabisa na hereni zile zinazovaliwa masikioni na wanawake na baadhi ya wanaume na yeye alibandika katika masikio yake yote mawili.

Walijidondosha sana

Licha ya Gendarmarie kuchapwa mabao manne kama si kujidondosha, huenda wangechapwa zaidi ya hayo au wao wangepata ya kufutia machozi.

Wachezaji wa kikosi hicho walikuwa kivutio kutokana na kitendo chao cha kujidondosha mara kwa mara na kusababisha mpira usimame kila baada ya dakika chache.

Hata hivyo, staili hiyo huenda walifikiri ni janja yao ya kupunguza idadi ya mabao kwani hata baada ya mchezo, kocha wao,

Mrundi Mvuyekure Issa aliweka wazi kuwa kabla ya kuanza mchezo walidhani wangepigwa mabao mengi zaidi ya hayo lakini kadri ya mchezo ulivyokwenda waliona tofauti.

Simba waanza na staili mpya

Kitaalamu timu zote zinatakiwa kila zinapomaliza kucheza mechi, zifanye mazoezi ya kutuliza misuli na sasa Simba imeanza staili hiyo ambayo wapinzani wao wa jadi Yanga walishaanza kitambo.

Simba waliitambulisha staili hiyo mara baada ya mchezo huo kumalizika ambapo walifanya mazoezi ya kukimbia kuuzunguka uwanja na baadaye walinyoosha misuli wakatoka.

Penalti ya Gendarmarie

Tukio la penalti ambalo Gendarmarie lingewakomboa na kupata bao la kufutia machozi, lakini cha kushangaza, uwezo wa mlinda mlango wa Simba, Aishi Manula aliyekuwa amejaa golini, uliwafanya wakose penalti hiyo.

Aishi alipangua penalti ya Gendarmarie iliyopigwa na Houssein Megane na kuwafanya watoke uwanjani hapo na kwenda kwao Djibouti watupu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here