SHARE

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda(pichani) ameagiza kukamatwa kwa mtu mmoja anayedaiwa kuhusika na tukio la kumbaka hadi kufa mtoto wa miaka mitano. Sambamba na hilo, pia ameagiza kukamatwa kwa kiongozi mmoja wa dini kwa kosa la kumkatisha masomo mwanafunzi wa Kidato cha Pili, kumzalisha watoto wawili na kumtelekeza.

Alitoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa kupokea Ripoti ya Malalamiko ya wananchi waliodhulumiwa haki zao ambapo zaidi ya wananchi 11,652 walijitokeza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Wananchi hao walifika katika ofisi hiyo ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kupata msaada wa kisheria uliotolewa kwa siku sita na jumla ya malalamiko 3,373 yalipokelewa na kusikilizwa huku wananchi waliosikilizwa wakiwa ni 6,052 Miongoni mwa changamoto zilizo wasilishwa kutoka kwa wanasheria hao ni pamoja migogoro ya ardhi, makosa ya jinai, mirathi, malezi ya watoto, madai, kulalamikia taasisi za kifedha na kibenki na kucheleweshwa kwa fidia.

Aidha Manispaa zote za jiji hilo zililalamikiwa kushindwa kutekeleza majukumu yake, mikataba ya mauziano kukiukwa, watendaji wa serikali za mitaa kuuza viwanja kimoja kwa mtu zaidi ya mmoja, kesi zinazoendelea mahakamani, Mahakama za Mwanzo kutotenda haki, na wananchi kukosa imani na Jeshi la Polisi na watendajiwa serikali.

Akizungumzia sakata la kubakwa hadi kufa kwa mtoto wa miaka mitano Mwanasheria Janet Eden alisema kuwa tukio hilo lilitokea mwaka juzi lakini hadi leo, Polisi wa Kituo cha Sitakishari Wilaya ya Ilala kulikoripotiwa kesi hiyo, wameshindwa kufungua kesi licha na kupewa taarifa za mtuhumiwa huyo huku mama wa mtoto akihangaika kupata haki yake.

Aliongeza kuwa hata mama wa mtoto huyo alipojaribu kumpeleka mtoto hosptali ili apatiwe matibabu, alinyimwa matibabu kwa kumhofia mtuhumiwa kitendo kilichosababisha mtoto huyo kufariki dunia. Baada ya kauli hiyo, Makonda aliagiza kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake na askari walioshindwa kuchukua hatua za kisheria kwa mtuhumiwa huyo, ili mlalamikaji apatiwe haki yake ya kisheria.

“Ni ajabu sana polisi anashindwa kumkamata mbakaji aliyembaka mtoto hadi kumsababishia kifo, kwa bahati mbaya mama yule hata hosptalini akanyimwa matibabu ya mtoto wake kwa kumhofia mtuhumiwa. “Hatuwezi kuwa na Polisi ambao wanaharibu sifa ya serikali, kituo cha Polisi Sitakishari ni lazima tupate majibu ya suala hili kwa kumkamata mtu huyu,” alisema Makonda.

Akizungumzia suala la kiongozi wa dini kumpa ujauzito binti wa Kidato cha pili Makonda alisema kwa mujibu wa taarifa iliyofikishwa kwa Mwanasheria na binti huyo ni kuwa alikuwa yatima na kiongozi huyo alikuwa akimsaidia ada lakini alimtaka kujihusisha naye kimapenzi ili amsaidie. Alisema, baada ya binti huyo kukubali ili asaidiwe alipata ujauzito na kiongozi huyo alimtelekeza binti huyo bila kumpa huduma yeyote.

Alisema, baada ya binti kupata tabu aliamua kurudi kwa kiongozi huyo ili amsaidie lakini alimtaka tena kujihusisha naye kimapenzi ili amsaidie kulea mtoto ndipo alipopata ujauzito wa mara ya pili lakini alipomtaarifu alimtolea kauli za vitisho na kumtelekeza. “Hawa viongozi wa dini tunaowaamini kwa ajili ya kufundisha maadili ndio wamekuwa wakiharibu waumini nataka atafutwe na afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake na binti huyu aliyeharibiwa maisha yake apate haki yake,”alisema Makonda.

Katika hatua nyingine Makonda amekosoa utendaji wa Mahakama ndani ya Mkoa huo na kusema kuwa ripoti imeonesha Mahakamani kugubikwa na dhuluma, kuchelewesha haki, na Mahakimu kuwatishia wateja wao. Malalamiko mengine ni kupotea kwa mafaili na nyaraka, kutumika kwa lugha ya Kiingereza katika kuendesha kesi jambo linalopelekea kuwanyima haki ya uelewa kwa washtakiwa na kukithiri kwa rushwa katika mhimili huo.

“Nawaza sijui niwapeleke wapi wananchi hawa wakapate haki kama taasisi nyeti ambazo zingesimamia haki zinawanyima haki. “Kuanzia serikali za mitaa hadi ngazi ya halmashauri wanaminya haki, Jeshi la Polisi wamepoteza imani nalo hali kadhalika Mahakama, sasa najiuliza nipeleke wapi kero za wananchi hawa zitatuliwe. Najua ni Mhimili unaojitegemea lakini kisitumike kigezo hiki kuwaumiza wananchi,”aliongeza.

Kwa upande wao wananchi walimshukuru Makonda kwa hatua alizochukua katika mkutano huo na kusema kuwa kupitia mkutano huo wameweza kujua mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya kisheria. “Tulikua na imani kubwa na Makonda na leo amedhihirisha ametusaidia wanyonge na ninaamini tutapata haki zetu kwa sababu tunauona mwanga, tunamshukuru sana,” alisema Bakari Mashoto mmoja wa wananchi waliokuwa na malalamiko ya kudhulumiwa ardhi. “Nimeitafuta haki kwa miaka zaidi ya saba nazungushwa tu lakini naziona dalili nzuri za kupata haki yangu asante Rais magufuli kwa kutuletea kiongozi anayethamini wanyonge,”alisema Happness Kinyaiya.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here