SHARE

SIMBA wajanja sana. Saa chache kabla ya kushuka Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam dhidi ya Gendermarie Nationale ya Djibout juzi Jumapili, kumbe tayari walikuwa na matokeo ya wapinzani wao wanaoweza kukutana nao raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, yaani El Masry ya Misri na Green Buffaloes ya Zambia.

Walishajua kuwa Waarabu wamepata ushindi mnono nyumbani wa mabao 4-0 dhidi ya maafande wa Zambia, wakaamua ngoja kwanza wamalize kazi yao kwa Wadjibouti kabla ya kuanza kudili na Wamisri hao wanaonolewa na Hossam Hassan.

Bahati nzuri Simba ikawajibu Waarabu kwa kuwatundika Wadjibouti kwa mabao 4-0 pia yaliyowekwa kimiani na Said Ndemla, John Bocco (mawili) na Emmanuel Okwi na kujiweka pazuri kukutana na El Masry.

Sasa unajua nini kilichotokea baada ya kumaliza gemu hiyo ya Uwanja wa Taifa? Fasta mabosi wa benchi la ufundi la Simba walijipa kazi ya kupitia mikanda na video kadhaa za mechi za Al Masry na kubaini jamaa si timu ya mchezo mchezo.

Hata hivyo katika kuchungulia huko, walibaini kuwa El Masry ina safu kali ya ushambuliaji ikiongozwa na Aristide Bance anayetokea Burkina Faso aliyefunga bao la pili wakati Wamisri hao wakiizamisha Green Buffaloes.

Pia waligundua kuna wakali wengine kama Ahmed Gomaa, Mohammed Grendo, Issouf Ouattara huku mabeki wake pia wakifunga kama hawana akili nzuri kwani katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Wazambia, Mohammed Koffi na Islam Salah ambao ni mabeki wa kati walitupia kambani kuonyesha walivyo na uchu.

Lakini, makocha wa Simba baada ya kubaini kuwa nao wana wachezaji wa nguvu na wenye kiu ya mafanikio, wakaangua kicheko cha furaha, kisha kuwaambia vijana wao ‘Hawa wanafungika bwana, tukiamua kukaza nje ndani’.

MSIKIE DJUMA

Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma, alisema wameiangalia El Masry wakiamini ndio wanaoweza kukutana nao katika mechi za raundi ya kwanza na kuamini licha ya ukali wao, Waarabu hao wanafungika kabisa.

Djuma alisema wanajua kama wakifuzu raundi ya kwanza watakuwa na mechi ngumu, lakini Simba inajiandaa kukabiliana na timu yoyote kwa vile nia yao ni kuona wanafika mbali kwenye michuano hiyo ili kujenga heshima ya soka lao Afrika.

“Tumewaona kupitia mikanda ya video, si timu ndogo. Tunajua wameshinda mabao 4-0 kama sisi, lakini tuna wachezaji mahiri ambao wana kiu ya kuweza kukabiliana na timu yoyote na tunaomba Mungu atusaidie,” alisema Djuma.

Djuma alisema kwa mabeki alionao kuanzia Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Juuko Murshid, Yusuf Mlipili na wengine wana uwezo mkubwa wakisaidiwa na kipa Aishi Manula, huku mbele wakijivunia kuwa na kina Bocco, Okwi na wenzao wakiwamo viungo wanaonyumbulika na kuiendesha timu kiushindi.

“Tunajua kadiri tunavyozidi kusonga mbele ndivyo tunavyokabiliana na timu ngumu, El Masry ina kikosi kizuri na inatoka kwenye nchi inayotamba katika soka Afrika, lakini hata sisi si wa kubezwa, tuna kikosi imara na kipana, tutapambana na Inshallah tutashinda,” alisema.

OKWI, BOCCO WALA KIAPO

Wakati huohuo, staa wa Simba, Emmanuel Okwi, ambaye ameifungia timu hiyo mabao 14 katika mashindano yote hadi sasa msimu huu, amefichua kuwa akiendelea kucheza sambamba na Bocco timu hiyo itakuwa ikivuna karamu ya mabao kwenye kila mchezo.

Okwi aliyewahi kucheza pia Yanga kwa muda mfupi mwaka 2014, alisema Bocco aliyeifungia Simba mabao 13 katika mashindano yote hadi sasa msimu huu, ni namba tisa asilia na ana uwezo wa kukaa na mpira, kutengeneza nafasi za kufunga na kuzifumania nyavu pia, hivyo wakiendelea kucheza pamoja watafanya vizuri.

“Tumekuwa na maelewano mazuri ya kimchezo kati yangu na Bocco na muda mwingi tumekuwa tukiangaliana na kupeana pasi za kufunga. Kwa hali hii nina imani tukiwa fiti katika kila mechi, tutaifungia timu yetu magoli mengi,” alisema Okwi.


1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here