SHARE

BAADHI ya wachambuzi wa siasa nchini wakiwemo wahadhiri, wamezungumzia uchaguzi wa mdogo katika majimbo ya Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakisema ulikuwa na upungufu wa wapigakura na wananchi walichagua mgombea na chama, badala ya sera.

Navyo vyama vya siasa vimepongeza ushiriki wa wananchi katika kupiga kura ili kupata wawakilishi watakaowaongoza na vimetaka wananchi sasa kuchapa kazi, kwa kuwa uchaguzi umekwisha na mshindi ameshapatikana.

Vyama vilivyoshiriki katika jimbo la Kinondoni ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), CCK, AFP, ADA TADEA, Chama cha Wananchi CUF, NRA, TLP, SAU na Demokrasia Makini.

Katika jimbo la Siha ni vyama vilivyoshiriki ni CCM, Chadema, CUF na SAU Wachambuzi Mchambuzi wa siasa, Profesa Mwesiga Baregu alisema uchaguzi huo, umeonekana kama maigizo na mambo yaliyofanyika, yalikuwa hayaeleweki. Alisema katika uchaguzi huo, wananchi waliojitokeza kupiga kura, walikuwa wachache chini ya mategemeo, hali inayofanya mtu ashindwe kujua Watanzania ni wa aina gani na maamuzi yao yasiyojulikana.

Alisema ipo haja ya kuchunguza, kwa nini watanzania hawakujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo. Alisema viashiria vinaonesha katika uchaguzi wa mwaka 2020, huenda kukawa na shida.

Profesa Baregu alisema jambo lingine la kujifunza katika uchaguzi huo wa Siha na Kinondoni ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo ilitakiwa kufanya mabadiliko ya msingi, kama vile kuhakikisha mawakala wanatafutwa na kuwepo vituoni kwa wakati, kwani ni watu muhimu wanaoweza kusababisha matokeo ya uchaguzi kukubalika au kubishaniwa. Pia, alisema Tume inatakiwa kuwa na mfumo thabiti unaohusu mawakala.

“Mawakala ndio wenye kutoa ushuhuda kuhusu mwenendo mzima wa uchaguzi, kwa mfano katika jimbo la Kinondoni kuna taarifa zilizoeleza kubebwa kwa sanduku la kura halafu likarudishwa huku uchaguzi ikiendelea,” alisema Profesa Baregu.

Kuhusu kampeni, Profesa huyo alisema zilikuwa za kistaarabu, ingawaje kufikia uchaguzi, jeshi la Polisi lilitumia nguvu kubwa isiyo na sababu. Alisema hali hiyo inaweza kuwa ni mojawapo ya vitu vilivyowaogopesha wananchi wengi kujitokeza kwa ajili ya kupiga kura.

Alisema ipo haja kwa jeshi hilo, kuangalia matumizi sahihi ya vyombo vya moto wanavyotumia na kufanya mabadiliko ya msingi.

Alisema hali ikiendelea hivi katika kila chaguzi, wapo watakaobakia wakinung’unika na wengine wakipata majeraha. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, alisema, uchaguzi ulikwenda vizuri, kwa kuwa wagombea wote walikuwa na hoja.

Alisema wapo wanasiasa waliingia katika uchaguzi huo, wakijiona bado wapo kwenye ‘chati’, lakini wamevuna walichokipanda.

Alisema CCM ilijaribu kuwaweka wagombea wawili waliotoka vyama vya upinzani, ambao walisema wanahama vyama vyao ili kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Alisema wagombea wote wawili wameshinda, lakini kama wasingeshinda, wangejilaumu kwa uamuzi wao. Aliongeza kuwa kilichoonekana katika uchaguzi huo, bado wananchi wana tabia ya kuwapigia kura watu na chama, hawaangalii sera.

“Katika uchaguzi huu ni ushahidi kuwa wananchi wengi wamemchagua mgombea na chama na si sera zake,“ alisema Bana.

Aidha, alisema katika chaguzi nyingi ndogo, kumekuwa na mwamko mdogo wa wananchi kujitokeza kupiga kura, kwa kuwa hakuna kitu kinachomlazimisha mwananchi kupiga kura.

“Uchaguzi huu umeonesha wananchi wanazikubali harakati na maamuzi serikali ya Magufuli hivyo rais anatakiwa kutembea kifua mbele kwa ushindi huu,” aliongeza Bana.

Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Alexander Makulilo alisema uchaguzi huo, unaonesha kuwa ipo haja kusimamia kanuni na taratibu ili watu wafanye siasa za kistaarabu.

Alisema vurugu zilizotokea juzi wilayani Kinondoni, hazileti picha nzuri kwa siasa za Tanzania. Alishauri wadau wanaohusika ikiwemo serikali, vyama vya siasa na taasisi zisizo za kiserikali, kuendelea kutoa elimu kwa umma ili wananchi watambue umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika chaguzi mbalimbali, zitakazowezesha kupata wawakilishi wanaowataka.

Vyama vya siasa

Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliwashukuru Watanzania hususani wananchi wa majimbo ya Kinondoni na Siha kwa kujitokeza kupiga kura na kuwezesha kupatikana kwa ushindi wa kishindo kwa zaidi ya wastani wa asilimia 70.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (CCM), Humphrey Polepole aliwashukuru wananchi wa majimbo hayo kwa kujitokeza kupiga kura ili kupata viongozi watakaowawakilisha, jambo ambalo ni heshima kubwa kwa chama hicho.

“Uchaguzi huo umeonesha kazi kubwa zilizofanywa na kukubalika na chama chetu kwa kushughulika na shida za wananchi, hivyo kwa ushindi huu tunawaahidi kuwa tutafanya kazi kwa bidii na hatutawaangusha,” alisema Polepole.

Hata hivyo, alivitaka vyama vya siasa, kujenga hoja na kuepuka malumbano, ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani. Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muhabi alisema mchakato mzima wa uchaguzi, ulikuwa na mapungufu yaliyoathiri vyama vya upinzani, ikiwa ni pamoja na mawakala kutopata taarifa kamili.

Hata hivyo, alisema mshindi ameshapatikana na uchaguzi umekwisha, hivyo kazi zianze kufanyika ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa majimbo hayo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji alishauri serikali kuwa ni heri iondoe mfumo wa vyama vingi kuliko kutokuwa na haki ya kugombea, ilhali wakiwa tayari na mgombea wao.

Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia alisema “Nawashukuru sana wananchi waliojitokeza kufanya haki yao ya kidemokrasia, pia naishukuru Tume ya Uchaguzi kwa umakini waliouonesha kuhakikisha tumefanya uchaguzi na kumaliza salama”.

Matokeo halisi Katika jimbo la Kinondoni, mgombea wa CCM, Mtulia alishinda kwa kupata kura 30,247 akifuatiwa na Salum Mwalim wa Chadema kura 12,353 na Rajab Salum wa CUF kura 1,943.

Vyama vingine vilivyosimamisha wagombea ni CCK, ADA TADEA, DP, NRA, UMD, TLP, AFP, SAU na Demokrasia Makini.

Kura ambazo wagombea wa vyama vingine walipata ni UMD 15, TLP 14, SAU 11, NRA 15, Demokrasia Makini 10, DP 21, CCK 129, AFP 12 na ADA TADEA 97. Wananchi waliojiandikisha kupiga kura katika jimbo hilo ni 264,055 ni waliopiga kura ni 45,454.

Kura halisi ni 44,867 na kura zilizoharibika ni 587. Baadhi ya kata zilizopo jimbo la Kinondoni ni Kigogo, Makumbusho, Kijitonyama, Kinondoni, Mburahati, Makurumla, Mabibo, Magomeni, Msasani, Mwananyamala, Ndugumbi, Tandale na Mzimuni.

Mtulia alihama CUF kwenda CCM Desemba 2, mwaka jana na Dk Mollel alihamia CCM Desemba 14, mwaka jana. Katika uchaguzi mkuu wa 2015, Mtulia aliyegombea kwa tiketi ya CUF, alishinda kwa kupata kura 70,337 wakati mgombea wa CCM wa wakati huo, Idd Azzan alipata kura 65,964.

Katika jimbo la Siha, mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Dk Godwin Mollel alipata kura 25,611 sawa na asilimia 80, akiwaacha mbali wapinzani wake, Elvis Mosi wa Chadema kura 5,905 sawa na asilimia 18.5, Tumsifueli Mwanri wa CUF kura 274 sawa na asilimia 0.9 na Mdoe Azaria wa SAU, aliyeambulia kura 170 sawa na asilimia 0.6 Jimbo hilo lina kata za Biriri, Gararagua, Karansi, Kashashi, Livishi, Makiwaru, Naeny, Nasai, Ndumet, Ngarenairobi, Olkolili na Sanya Juu.

Wananchi waliojiandikisha kupiga kura katika jimbo hilo la Siha ni 55,313 na waliopiga kura ni 32,277.

Idadi ya kura halali ni 31,960 na kura zilizokataliwa ni 317. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Polisi mkoani Kilimanjaro walitoa shukrani za dhati kwa wananchi wote, waliojitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu ili kupata viongozi wao kwa njia ya kidemokrasia.

@Habari leo

 


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here