SHARE

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Ngorongoro mkoani Arusha kimeendelea kupasuka baada ya Mwenyekiti wake wa Wilaya na wanachama zaidi ya 307 kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baada ya kujiengua Chadema na kujiunga CCM wakiwa na Mwenyekiti wao wa wilaya, Simon Ole Ndekubare na aliyekuwa mgombea udiwani katika Kata ya Piyaya, Yohana Kerenge, wanachama hao waliapishwa mbele ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Lootha Sanare kiapo cha utiifu na kupewa kadi mpya za CCM na mwenyekiti huyo.

Akizungumza baada ya kuapishwa na kupewa kadi mpya, Ole Ndekubare alisema alikuwa katika chama hicho, lakini hakuwa na kadi wala ofisi na fedha zote za ruzuku zaidi ya Sh milioni 500 zinatumika na baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho.

Alisema alikuwa akifanya kazi katika mazingira magumu kwa kipindi kirefu yeye na viongozi wenzake na uamuzi aliofanya na kundi la wanachama wa Chadema, uko sahihi na kamwe hawatajutia.

Ndekubare alisema kurudi CCM ni uamuzi uliofanywa kwa kuzingatia mambo mengi ikiwamo kukumbwa na upepo bila kujitafakari na pia utendaji kazi wenye kasi unaofanywa na Rais John Magufuli.

“Watu watasema mengi, lakini nimeamua mimi na kundi langu kurudi CCM.Sasa wenye kusema waendelee kusema, lakini Chadema Ngorongoro imekufa hakuna tena kiongozi amebaki katibu wa wilaya tu,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Sanare aliwashukuru wanachama hao wa Chadema kwa kurudi CCM na kukubali utendaji kazi wa Rais, na kwamba waliobaki Chadema iko siku tu wataamua kurudi nyumbani maana CCM ni chama pekee chenye demokrasia ya kweli.

Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, William Ole Nasha aliwataka wanaChadema waliobaki huko kuamua haraka kurudi CCM na uamuzi wao hawataujutia.

Aliwataka waliorudi CCM kuwa wamoja na kujijenga chama hicho kwa maslahi ya wanachama na kuvunja makundi yasiyokuwa na maana.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ngorongoro, Amos Shimba alimwambia Mwenyekiti wa CCM Mkoa, kuwa mbali ya hao 307 waliojiunga kutoka Chadema, kuna wanachama wengine 173 walisharudi na kupewa kadi siku za nyuma.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here