SHARE

MBUNGE katika Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu amesema, lugha ya Kiingereza inamsumbua kuelewa kile kinachozungumzwa bungeni.

Mbunge huyo, Hillary Rono ambaye ni mwakilishi katika Kata ya Kipkenyo, alilazimika kukatisha hotuba ya mbunge mwenzake wa Viti Maalumu, Jenny Too.

Baada ya kuona haambulii chochote katika hotuba ya Mbunge Too, alimwomba Spika amwagize mwakilishi huyo wa Viti Maalumu kuondoa misamiati ya Kiingereza na kuweka maneno rahisi ili aweze kuelewa.

Umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili ulionekana baada ya wabunge wengine kuunga mkono hoja ya Rono kuonesha kuwa hata wao Kiingereza cha Mbunge mwenzao kilikuwa tatizo kwao.

Kwa umoja wao kupitia kwa Spika wa Bunge hilo walimshurutisha Mbunge Too kuwaomba radhi wenzake kwa kutumia misamiati migumu.

Tukio hilo la kipekee nchini Kenya lilitokea mwishoni mwa wiki na kuwaacha wabunge wengine walioelewa Kiingereza cha Too wakiwa hoi kwa vicheko.

Too, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa mkongwe na machachari kupitia chama cha KANU marehemu Mark Too, alianza kulalamikiwa mapema baada ya kuanza salamu yake kwa spika na wabunge wote. Rono alilazimika kutumia nguvu ya ziada baada ya maombi yake ya tangu awali kutosikilizwa na spika.

Baada ya spika kuona umuhimu wa kutumia lugha rafiki bungeni ili kuwa rahisi kwa wabunge wote aliamua kuisikiliza hoja ya Rono. Rono akasema kuwa ni tabia ya mbunge Too kutumia lugha ngumu huku akijua kuwa wenzake wanasumbuka kumwelewa.

Spika wa Bunge, David Kiplagat akaingilia kati na kumwomba Too atumie lugha rafiki kwa wabunge wote. Malalamiko hayo yamekuja wakati mbunge Too alipokuwa akichangia muswada wa sheria kuhusu usalama wa chakula nchini.

Katika hotuba yake ambayo ililalamikiwa na baadhi ya wabunge kuwa ilitolewa kwa lugha ambayo haikuwa rafiki kwa wabunge, Too aliunga mkono muswada kutokana na mateso anayoyaona kwa wananchi wa Kenya.

“Nimemkumbuka mwananchi mmoja masikini anayepanda kabichi pembeni ya mto na kuziuza maeneo ya Kiambu,” alisema Too katika mchango wake na kuongeza;

“Spika ili tuweze kuwajali wakulima wote hasa wanawake ambao ndio wanaokamua maziwa, wanaoishi kwa ulemavu na kwenda sokoni kutafuta riziki ya familia, lazima tuwe na usalama wa chakula.”

Kabla hajamaliza mchango wake, Rono alimkatiza na kuomba mwongozo, “Mheshimiwa Spika, mbunge Jenny Too kiingereza chake ni cha haraka sana hadi sisi wabunge wengine hatuelewi kuwa anasema nini”.

Kutokana na hali hiyo katika Bunge la Uasin Gishu, unaweza kuona kuwa lugha rafiki ambayo inaweza kutumika na kutoleta minung’uniko nchini Kenya ni Kiswahili pekee kwa sababu kinaeleweka kwa wananchi walio wengi nchini humo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here