SHARE

SERIKALI imepeleka sh. bilioni 1.92 katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wilayani Mtwara kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya.

Hayo yalibainika jana wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozungumza na wakazi wa Halmashauri hiyo, wakati wa ziara yake.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi alisema fedha hizo zilitolewa na Serikali ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Alisema jumla ya sh. bilioni 1.2 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kwenye Kata ya Njengwa, ambapo aliwasisitiza watendaji kutobadilisha matumizi.

Waziri Mkuu alisema ujenzi huo utahusisha chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume, eneo la kuchomea taka na chumba cha kuhifhadhia maiti.

“Serikali imeamua kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao.”

Aidha, Waziri Mkuu aliwataka wananchi hao kuendelea kuiunga mkono Serikali yao, ambayo imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.

Pia Waziri Mkuu alisema Serikali inatarajia kuipitia upya sheria ya elimu pamoja na sheria ya mtoto ili kuweka masharti ya kumlinda mtoto wa kike hususani kudhibiti mimba kwa wanafunzi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Gelasius Byakanwa alisema Serikali itawachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwapa watoto wa kike dawa za uzazi wa mpango ili kuwazuia wasipate mimba.

Bw. Byakanwa alisema wanafunzi wa kike katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wamebainika kuwa wanatumia dawa za kuzuia mimba wakiwa shuleni, hivyo kuwaruhusu kushiriki katika matendo yasiyokuwa ya kimasomo.

Alisema Serikali itafanya msako wa kuwatafuta wote wanaotumia dawa hizo pamoja na wanaowapa na watakaobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa sababu jambo ni hatari kwa maendeleo ya wanafunzi hao.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Josephat Kakunda alisema alisema Serikali imepeleka sh. bilioni 1.92 katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ili kuboresha huduma za afya.

Asema kati yake sh. milioni 700 zilipelekwa katika kituo cha afya cha Nanyamba ambapo sh. milioni 300 zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa dawa na sh milioni 400 ukarabati wa kituo, huku sh. bilioni 1.2 ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Njengwa.

Haya hivyo, Waziri huyo alisema kuwa Serikali inampango wa kuifanyia marekebisho sheria ya mtoto kwa kuondoa kipengele cha dhamana kwa watu watakaotuhumiwa kuwapa mimba watoto wa shule.

Alisema hatua hiyo inatokana na baadhi ya watuhumiwa hao wanapopewa dhamana kwenda kuzungumza na wazazi au walezi wa binti jambo linalochangia katika kuharibu ushahidi.” Ni bora wakakaa rumande hadi hukumu itakapotolewa na kama hawatokutwa na hatia watarudi uraiani”.

 


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here