SHARE

KILA mtihani una swali gumu la kujibu. Ni kama swali la kama Simba inaweza kuitoa Al Masry kwao Misri katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.

Rekodi za miaka ya nyuma zinaigomea Simba kwani haijawahi kupata ushindi wowote ugenini dhidi ya timu kutoka Ukanda wa Afrika Kaskazini. Watoto wa mjini wanapenda kuwaita Waarabu.

Iliwahi kwenda kucheza na Ismailia na Zamalek za Misri lakini ikafungwa. Bahati nzuri, Simba ilifungwa bao 1-0 na Zamalek na ilikuwa imepata ushindi kama huo nyumbani hivyo mechi ikaamuliwa kwa mikwaju ya penalti na Simba ilipeta. Ila ndani ya dakika 90, Simba ilichezea kichapo.

Simba iliwahi pia kwenda kucheza na Haras El Hadood na Es Setif ikafungwa.

Iliwahi pia kwenda kucheza na Al Ahly ikafungwa. Simba haijawahi kuifunga timu yoyote ya Kiarabu kwao, labda hii iwe mara ya kwanza.

Awamu hii matokeo ya nyumbani yalikuwa sare ya mabao 2-2 hivyo Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele. Inawezekana? Ni jambo gumu kusema.

Makala haya yanaangazia mambo matano ambayo yataamua mchezo huo wa marudiano ambao utachezwa Jumamosi ya wiki hii na Mwanaspoti litakuwa moja kwa nchini humo kukuletea mfululizo wa matukio yote.

OKWI, BOCCO VIWANGO

Kitu cha kwanza ambacho kinaweza kuamua mchezo huo ni kiwango cha mastaa wawili wa Simba, John Bocco na Emmanuel Okwi.

Mastaa hao wawili mpaka sasa wamefunga mabao 36 katika mashindano yote. Msimu huu ndio wamekuwa wakombozi wa Simba.

Okwi na Bocco ndio waliofunga mabao ya mchezo wa kwanza, na kwa ujumla wamefunga mabao sita katika michuano hiyo mpaka sasa. Kila mmoja amefunga matatu.

Kwenye mchezo wa kwanza, Okwi alicheza kwa kiwango bora lakini Bocco alikuwa chini kidogo kutokana na kuwa na maumivu. Alifanyiwa mabadiliko kipindi cha pili.

Kwenye mchezo huo nguvu ya Okwi na Bocco katika kukaba kuanzia mbele, pamoja na ujanja kwenye kufunga vinaweza kuamua mechi.

Ikumbukwe Simba inahitaji kufunga mabao ili kushinda mchezo huo.

BEKI YA KATI

Eneo jingine ambalo litaamua kama Simba inashinda mchezo huo ama la, ni beki yao ya kati. Kocha wa Simba, Pierre Lechantre atalazimika kuifanyia mabadiliko kidogo beki hiyo hasa kutokana na makali ya safu ya ushambuliaji ya Al Masry.

Beki Mganda, Juuko Murshid ni lazima acheze kwenye mchezo huo wa marudiano kama Simba inataka kupunguza dhahama ya kufungwa.

Juuko amekuwa akicheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Uganda na mwaka jana alicheza mechi mbili dhidi ya timu ya taifa ya Misri ambapo waliruhusu bao moja tu.

Ni wazi kwamba ana uzoefu mkubwa wa kuwakaba washambuliaji wasumbufu hasa kutoka Misri.

Erasto Nyoni anacheza vizuri lakini anahitaji kucheza kwa akili kubwa kwani washambuliaji wa Al Masry wanamzidi kasi hivyo wakimwacha tu itakuwa ni kilio.

NGUVU YA MKUDE, KOTEI

Pamoja na kwamba beki ya kati ya Simba inahitaji utulivu mkubwa, bado kiwango cha viungo wake wawili, James Kotei na Jonas Mkude kina nafasi ya kuamua matokeo ya mchezo huo.

Viungo hawa ndio wanaopunguza hatari katika lango la Simba. Wanatakiwa kuwa fiti kwa dakika zote. Wanatakiwa kuwa imara katika kupokonya mipira pia kusaidia kwenye umiliki wa mpira kwa timu yao.

Makosa mengi katika safu ya kiungo yatapelekea Simba kupoteza mchezo huo. Mkude na Kotei wameushika mchezo huo.

Pia Shomary Kapombe ambaye anatarajiwa kucheza kwenye kiungo anatakiwa kusaidiana na wakali hao katika kusaidia Simba isiruhusu hatari nyingi langoni mwao.

MBINU ZA LECHANTRE

Wachezaji wanaweza kujituma kwa kiwango cha juu lakini kama kocha mkuu atakuwa na mbinu hafifu, uwezekano wa kushinda ni mdogo.

Hapa ndipo anapoingia Lechantre. Kocha huyo Mfaransa ana uzoefu na soka la Afrika Kaskazini na anatakiwa kuonyesha hilo kwenye mchezo wa marudiano.

Lechante ataamua mchezo huo kuanzia namna anavyokipanga kikosi chake, mfumo atakaoutumia na mabadiliko ya ndani ya uwanja atakayofanya. Kosa moja tu Simba inaweza kufungwa kirahisi.

MZIKI WA GOMAA, BANCE

Pamoja na yote, uwezo mkubwa wa nyota wa Al Masry kama Ahmed Gomaa, Ahmed Shoukry, Mohammed Mahmoud, Aristide Bance ndio utakaoamua mchezo huo.

Nyota hao walisumbua vilivyo kwenye mchezo wa kwanza hivyo watakuwa moto pia kwenye mchezo wa marudiano. Ni wachezaji wajanja wajanja na wenye kulazimisha mambo.

Beki ya Simba ikizubaa kidogo nyota hao wanaweza kuamua mchezo huo. Simba inahitaji nguvu kubwa kuwazuia kwa dakika 90.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here