SHARE

MUUNGANO wa Jamii Tanzania (Mujata), umeiomba serikali kuingilia kati na kupiga marufuku watu wanaoendelea kueneza imani “potofu ya Freemason” nchini kwa madai kuwa inachochea vitendo vya kihalifu, yakiwamo mauaji

Ombi hilo lilitolewa jijini Mbeya na Mwenyekiti wa Mujata Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Chifu Shayo Masoko, wakati wa mkutano maalumu wa umoja huo unaowaunganisha viongozi wa dini, mila na serikali.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wa Mujata kutoka katika Kanda mbalimbali za umoja huo nchini pamoja na viongozi wa mila na dini kutoka nchi jirani za Kenya, Malawi na Zambia.

Wageni hao walikuwa waalikwa kwa ajili ya kuimarisha ujirani mwema.

Chifu Masoko alisema imani hiyo ya “Freemason” inawachochea vijana na watoto nchini kuamini kuwa ili mtu atajirike ni lazima amwage damu za watu hivyo kuwa na uwezekano wa kushiriki vitendo viovu vya mauaji.

“Tunashangaa serikali kuendelea kukaa kimya bila kutoa tamko lolote la kukemea juu ya imani ya Freemason ambayo inawafanya vijana kushiriki vitendo vya mauaji,” alisema chifu huyo. “Imani hii (potofu) inawaaminisha vijana kuamini kuwa Freemason ni mtu aliyevuna utajiri kutokana na kumwaga damu za watu,” alisema Chifu Masoko.

Aliomba serikali kuungana na umoja huo kupiga vita imani hiyo kama ilivyofanya kwenye vita dhidi ya mauaji ya watu wenye ualbino hasa katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Mbeya pamoja na kutokomeza vitendo vya uchunaji wa ngozi katika Wilaya ya Mbozi.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, aliupongeza muungano huo kwa kuisaidia serikali kupambana na maovu yanayoweza kuhatarisha amani kwenye jamii.

Alisema kitendo cha kuwashirikisha viongozi wa muungano huo kutoka katika Kanda mbalimbali kitasaidia kuzuia vitendo vya uhalifu kuhama kutoka mkoa mmoja kwenda katika mwingine kwa madai kuwa tabia ya vitendo viovu huigwa.

Februari 26, mwaka huu Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilimkamata Rajabu Mohammed (25), maarufu kama Rajesh, ambaye alikuwa akiwatishia wanawake kuwa ni ‘Freemason’ ili wampe mali walizonazo na kisha kuwaingilia kimwili.

Akizungumza na waandishi wa habari siku hiyo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Mwenge alikamatwa siku tatu nyuma Kinondoni.

Alisema Rajab alikuwa akifanya uhalifu huo kwa kutumia gari lake aina ya Toyota Fun Cargo lenye namba za usajili T172 BLH rangi ya fedha.

VITU VYAOAkisimulia namna wanawake walivyoingia kwenye mtego wa mtuhumiwa huyo, Kamanda Mambosasa alisema Mohammed na wenzake walikuwa wakiwakamata wanawake na kuwaingiza kwenye gari hilo kwa nguvu.

“Huwakamata wanawake kwa kuwalaghai kuwa ni wafanyabiashara na wakishaingia kwenye gari la huyu mtuhumiwa wananyang’anywa vitu vyao na wamekuwa wakiwatishia kuwa ni Freemason,” alisema na kueleza zaidi:

“Huwatishia kuwaua kwa kuwanyonya damu au kuwakata sehemu zao za siri; kupitia vitisho hivyo huwalazimisha watoe namba za siri za simu zao na kuchukua kadi za benki na kuwaibia fedha kwenye ATM.

“Huyu anafanya mchezo huu kwa kushirikiana na wenzake ambao bado tunawasaka.”

Alisema baada ya kuwaibia fedha wana kawaida ya kuwapeleka sehemu na kuwafanyia vitendo vya kikatili, ikiwemo kuwaingilia kimwili.

“Huyu kijana ni mbaya sana amekuwa akiwafanyia vitendo vya unyanyasaji… matendo ambayo siwezi kuyataja hapa naona aibu. Lakini nadhani mmenielewa. Anaona haitoshi, anawabaka.

“Tumemhoji amekiri kufanya hivyo na anadai ameacha, hivi unaweza kusema umeacha? Je, kama una ukimwi umeusambaza kwa wanawake wangapi?” Alihoji kamanda huyo.

“Tunaendelea na upelelezi na kuwasaka aliokuwa akishirikiana nao. Mpaka sasa malalamiko yaliyofunguliwa kituoni ni ya wanawake watatu.”

Kamanda Mambosasa aliomba wanawake ambao wamefanyiwa unyanyasaji na mtuhumiwa huyo wajitokeze kwenye vituo vya polisi.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here