SHARE

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amebainisha mambo saba yaliyoathiri utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/18.

Akiwasilisha kwa wabunge mapendekezo ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2018/19 mjini hapa jana, Dk. Mpango alisema malimbikizo ya madai serikalini ni miongoni wa mambo yaliyoathiri utekelezaji wa bajeti hiyo iliyobakiza miezi mitatu kufika ukomo.

Waziri huyo alitaja mambo mengine kuwa ni pamoja na ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji, matayarisho hafifu ya miradi na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya usafiri kutokana na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo.

Kiongozi huyo wa serikali alizitaja changamoto nyingine kuwa ni mwamko mdogo wa kulipa kodi hususan kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki, masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo ya kibiashara kutoka nje na mabadiliko ya sera za misaada katika nchi zilizokuwa zikiipatia Tanzania msaada wa kibajeti.

Machi 28, mwaka jana, Dk. Mpango wakati akiwasilisha mapendekezo ya ukomo wa bajeti serikali kwa mwaka 2017/18 alibainisha changamoto tano zinazoathiri utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 iliyokuwa ya Sh. trilioni 29.539 na karibu zote zimeonekana kujitokeza tena katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Alisema kuwa katika mwaka huo wa fedha, serikali ilipanga kutumia Sh. trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 8.702 zilikuwa za ndani na Sh. trilioni 3.117 za nje, lakini hadi kufikia Februari mwaka jana, fedha za miradi ya maendeleo zilizokuwa zimetolewa na serikali ni Sh. trilioni 3.975 ikijumuisha fedha zilizotolewa kwa halmashauri, sawa na asilimia 34 ya bajeti yote ya maendeleo.

Waziri huyo alisema kiwango hicho kidogo cha fedha za maendeleo kilichotolewa kilisababishwa na vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuelekeza sehemu ya fedha kulipia madeni ya miradi ya maendeleo.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo kutokana na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu na kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha kimataifa.

Waziri huyo alitaja sababu nyingine ya kutotekelezwa kwa kiwango kikubwa kwa bajeti ya maendeleo na mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2016/17 kuwa ni matayarisho hafifu ya miradi na mwamko mdogo wa kulipa kodi hususan uzingatiaji wa matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).

Ili kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa, Dk. Mpango alisema serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana nazo kwa kuhakikisha fedha zinaelekezwa kwenye miradi yenye tija na kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara, ili kuvutia uwekezaji nchini.

JANUARI MWAKA HUUKatika uwasilishaji wake jana, waziri huyo alisema mwenendo wa mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18 ambao serikali ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh. trilioni 31.712, unaonyesha kuwa hadi kufikia Januari mwaka huu, jumla ya mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia Sh. trilioni 17.4, sawa na asilimia 85 ya lengo.

Alifafanua kuwa kati yake, mapato ya kodi yalikuwa Sh. trilioni 10.03, sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 11.36.

“Mapato yasiyo ya kodi yalikuwa Sh. trilioni 1.45, sawa na asilimia 98.2 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.48, mapato yaliyokusanywa na halmashauri yalikuwa Sh. bilioni 345.9, sawa na asilimia 74.1 ya makadirio ya Sh. bilioni 466.9,” alisema.

Dk. Mpango alisema misaada ya mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ilifikia Sh. trilioni 1.4 sawa na asilimia 66 ya lengo la kupata Sh. trilioni 2.14, mikopo ya ndani ilifikia Sh. trilioni 3.93 ikiwa ni asilimia 95.6 ya kiasi kilichopangwa kukopwa ikijumuisha Sh. trilioni 3.24 zilizokopwa kulipia amana za serikali zilizoiva na mikopo mipya ya Sh. bilioni 685 na mikopo ya nje ya kibiashara ilifikia Sh. bilioni 224.1.

Dk. Mpango alibainisha kuwa katika kipindi hicho serikali ilitoa mgawo wa Sh. trilioni 17.4 kwa mafungu mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti, sawa na asilimia 85 ya makadirio ya bajeti.

“Kati ya kiasi hicho, Sh. trilioni 13.34 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 4.05 kwa matumizi ya maendeleo, zikijumuisha Sh. trilioni 3.44 za ndani na Sh. bilioni 604.5 za nje,”alisema Dk. Mpango.

MAENEO VIPAUMBELEAliyataja maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mgawo wa bajeti hiyo kuwa ni pamoja na kulipa deni la serikali na mishahara ya watumishi wa umma, kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege na kulipa malimbikizo ya madai ya wazabuni, makandarasi na watumishi wa umma.

Utekelezaji wa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme, kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, kugharamia elimu msingi bila ada, utekelezaji wa miradi ya maji na kununua vifaa tiba pia ulipewa kipaumbele.

Waziri huyo alisema mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa bajeti hiyo ni pamoja na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, akibainisha kuwa jumla ya Sh. bilioni 59 zilitolewa kwa halmashauri za wilaya 110 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.

Alisema Sh. bilioni 24.1 zilitolewa kwa ajili ya ukarabati wa hospitali za mikoa 24 na Sh. bilioni 125.7 zikitolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

“Katika kutekeleza lengo la kuwapatia wananchi mijini na vijijini huduma ya maji safi na salama, kiasi cha Sh. bilioni 149.3 kilitolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, pia usambazaji wa umeme Sh. bilioni 300.9 kwa ajili ya miradi ya nishati vijijini, joto ardhi, uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo mbalimbali na usambazaji wa gesi asilia,” alisema Dk. Mpango.

Alisema mafanikio mengine ni kufikiwa kwa azima ya kutoa elimu bila ada na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu akibainisha kuwa serikali imetoa Sh. bilioni 543.5.

Dk. Mpango pia alisema serikali imeendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu, ili kupanua fursa za uchumi, kilimo na viwanda zikiwamo barabara zinazounganisha mikoa na nchi jirani, zinazopunguza msongamano katika majiji, barabara za vijijini, reli, viwanja vya ndege na bandari, Sh. trilioni 1.451 zikitolewa.

“Malimbikizo ya madai ya watumishi umma, wazabuni, makandarasi na watoa huduma yameshughulikiwa ambapo kiasi cha Sh. bilioni 939.5 kimelipwa,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here