SHARE

Wakati Simba wakiwa ondoka leo kuelekea Misri tayari kwa mchezo wa marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Masry, wametakiwa kuwa makini na fitna za Waarabu hao.

Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza, uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mashindano hayo ya kimataifa.

Baadhi ya nyota wa zamani wa Simba ambao walikuwa kwenye kikosi cha timu hiyo ambayo iliweka rekodi ya kuiondoa Zamalek, 2003 kwa mikwaju ya penalty wamezitaja fitna ambazo alikutana nazo na kuwasisitiza viongozi kuwa makini nchini humo.

Simba itacheza mchezo wake wa pili wa marudiano dhidi ya Al Masry nchini Misri, Machi 17 kwenye uwanja wa Ismaïlia majira ya saa 2:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Ulimboka Mwakingwe amesema moja ya fitna ambazo waarabu walizifanya dhidi yao ni kuwazungusha umbali mrefu kwa lengo la kuwachosha na kusababisha malumbano baina yao.

“Tulienda kama awamu tatu au nne hivi, lakini jamaa wamekuwa na mbinu nyingi za kuwaondoa wachezaji mchezoni, nakumbuka tuliwahi kukutana na kasumba ya kufikia eneo ambalo lilikuwa na upatinaji mkubwa wa kina dada wanao fanya biashara haramu ya miili yao.

“Katika mazingira kama hayo unakuta badala ya wachezaji kuelekeza mawazo yao kwenye mechi wanaanza kupagawa na hao wanawake, hili wanatakiwa kuwa nalo makini japo zaman azo zimebadilika,” alisema Ulimboka.

Ameendelea; “Simba inatakiwa kuwa na watu wao wa kuwaongoza ili yasiwakute yale ambayo yalitokea kwenza zama zetu,vyakula na mengineyo nayo wanatakiwa kuyatizama kwa macho ya tofauti.”

Victor Costa “Nyumba” amesema wachezaji wa Simba wanatakiwa kujitoa kwa asilimia zote kwenye mchezo huo ili kuweza kuwaondoa Al Masry.

“Kuwaondoa kwetu Zamalek kulichangiwa sana na kuwa kwetu kitu kimoja,fitna tulikutana nazo na kwa ufupi ni lazima Simba watambue kuwa Waarabu hawana fitna moja, kama wakijipanga na hii basi watakutana na nyingine.

“Kikubwa ni kuwa tayari kwa lolote ambalo litakuwa mbele yao, kuwahi kwao mapema kutawasaidia kujua mazingira na vinginevyo lakini kama wakichelewa itawapa wakati mgumu kuvikwepa vigingi vya fitna zao,” alisema beki huyo wa kati.

Boniface Pawasa ameitaka Simba kuwa na mipango madhubuti ya kimbinu ambayo itaendana na namna ambavyo Waarabu wamekuwa wakicheza.

“Masuala ya fitna ni kawaida yao lakini makocha wa Simba pamoja na jopo lao la viongozi kila mmoja kwa nafasi yake wanatakiwa kujikita zaidi kwenye majukumu yao.

“Ukicheza na Mwarabu unatakiwa kuwa na nidhamu kubwa ya mchezo kwa maana ya kutocheza rafu zisizo na msingi,wale ni wepesi wa kumtafutia mtu kadi ili mpungue pia ni wepesi kukupanikisha kwa kufanya matukio ya chini kwa chini.

“Al Masry hawana mpira wa ajabu lakini wanauwezo mzuri wa kufunga, umakini kwenye kujilinda unatakiwa kuongezeka kwa Simba,” alisema Pawasa.

Emmanuel Gabriel ambaye alikuwa mshambuliaji amesema benchi la ufundi linatakiwa kuhakikisha kikosi kinakuwa kwenye hali nzuri kwa maana ya molali ya wachezaji.

“Ugenini ni kugumu, kitakachoweza kusaidia pekee ni kuwapandisha wachezaji molali ili wacheze kwa kujituma,tulionyesha kuwa inawezekana kinachotakiwa ni kuendeleza kile ambacho tulikifanya,” alisema Gabriel.

Naye Amri Said ambaye kwa sasa ni kocha wa Lipuli, amesema ubora wa Simba hasa kwenye safu yake ya ushambuliaji unaweza kuwasaidia kupata mabao nchini Misri.

“Sina maana kuwa Simba hii ni bora kuliko ile, ukiangalia kipindi kile tulikuwa na Ramadhani Waso pekee kama mchezaji wa kigeni,walio salia ni wazawa waliokuwa na uwezo mkubwa na mioyo yakujitolea zaidi.

“Wageni wanaondoa ile hali ya uzalendo wa upambanaji ni wachache ambao wanacheza kwa moyo, lakini pamoja na yote bado Simba inaweza kushinda mchezo huo na kusonga mbele,” alisema kocha huyo wa Lipuli.

 


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here