SHARE

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, Jumanne alikamatwa na kuwekwa korokoroni ikiwa ni sehemu ya uchunguzi kwamba alipokea mamilioni ya euro kinyume cha sheria kutoka utawala wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gadafi.

Ofisa mmoja wa mahakama anayelijua vyema tukio hilo aliiambia shirika la The Associated Press kuwa Sarkozy alishikiliwa katika kituo cha polisi cha Nanterre, magharibi mwa Paris.

Ofisa huyo alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake kwa vile hakuwa na mamlaka ya kujadili jambo hilo hadharani.

Taarifa zinasema Sarkozy pamoja na mkuu wake wa zamani wa utawala wamekana shtaka dhidi yao katika kesi hiyo ambayo inahusisha gharama za kampeni zake za urais alioshinda mwaka 2007.

Ingawa uchunguzi umekuwa ukifanyika tangu mwaka 2013, kesi hiyo ilipata msukumo miaka mitatu baadaye wakati mfanyabiashara mwenye asili ya Ufaransa na Lebanon, Ziad Takieddine alipoiambia tovuti ya uchunguzi mtandaoni, Mediapart, kwamba alipeleka kwa Sarkozy na mkuu wa zamani wa wafanyakazi, Claude Gueant masanduku yenye fedha taslimu Euro 5 milioni (Dola 6.2 milioni za Marekani) yaliyotoka Libya.

Mwanasheria wa Sarkozy hakujibu mara moja ujumbe kutoka kwa AP ambao ulikuwa unataka maoni yake.

Wachunguzi wanafuatilia madai kwamba serikali ya Gadafi kwa siri ilimpatia Sarkozy jumla ya Euro 50 milioni kwa ajili ya kampeni za uchaguzi wa mwaka 2007.

Kiasi hicho ni zaidi ya mara mbili ya kikomo cha fedha za kampeni kisheria ambacho ni Euro 21 milioni.

Aidha, malipo hayo yanayodaiwa yatakuwa yamekiuka sheria za Ufaransa zinazokataza fedha za kigeni kuingizwa na zinazotaka kutangaza chanzo cha fedha za kampeni.

Katika mahojiano na Mediapart yaliyochapishwa Novemba 2016, Takieddine alisema alipewa Euro 5 milioni Tripoli na mkuu wa intelejensia wa Gadafi wakati wa safari mwishoni mwa mwaka 2006 na 2007 na kwamba, alimpatia fedha zikiwa katika masanduku Sarkozy na Gueant mara tatu.

Alisema makabidhiano yalifanyika katika Wizara ya Mambo ya Ndani, wakati Sarkozy alikuwa waziri wa wizara hiyo.

Takieddine kwa miaka kadhaa amejikuta kwenye matatizo yeye mwenyewe na vyombo vya haki vya Ufaransa yaliyojikita hasa katika madai kwamba alitoa fedha kinyume cha sheria kwa kampeni za mwanasiasa wa kihafidhina Edouard Balladur kwa ajili ya uchaguzi wa rais mwaka 1995 – zilizotokana na kamisheni ya uuzaji wa nyambizi za Kifaransa kwa Pakistan.

Kwa mujibu wa gazeti la Le Monde, wachunguzi katika siku za karibuni waliwapa mahakimu ripoti ambayo wamefafanua jinsi fedha zilivyozungushwa ndani ya timu ya kampeni ya Sarkozy.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here