SHARE

MAPENDEKEZO yaliyotangazwa na Jumuiya ya Mabenki Tanzania ya kushusha riba za mikopo kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia sita kwa benki za biashara nchini, yameelezwa kuwa yataleta neema kwa uchumi wa Tanzania.

Azma hiyo ya kushusha riba ilitangazwa kwenye Mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Ikulu Dar es Salaam Jumatatu wiki hii chini ya uenyekiti wa Rais John Magufuli. Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika Ikulu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki, Dk Charles Kimei alimweleza Rais Magufuli na wajumbe wengine kuwa riba ya mikopo katika benki za biashara hapa nchini imeshuka kwa asilimia 16 kutoka asilimia 22.

Kwa mujibu wa Dk Kimei, jambo lililosababisha kuwepo kwa riba kubwa kwa wafanyabiashara kulitokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoza riba kubwa kwa benki zilizokuwa zikikopa kutoka BoT. Wataalamu wa uchumi waliozungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu jana walisema faida sita zitakazopatikana kama mpango huo utatekelezwa ni kuwepo kwa ongezeko la mikopo, ongezeko la wakopaji, na ongezeko la biashara. Faida nyingi ni ongezeko la makusanyo ya kodi, ongezeko la ajira kwa wananchi masikini na ongezeko la miradi ya maendeleo katika sekta zote muhimu ikiwemo za elimu, afya na uchumi.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi alisema kuwa mpango wa kushushwa kwa riba hiyo hadi kufikia asilimia sita kutachochea idadi ya wakopaji kuongezeka kwa kuwa itakuwa rahisi kwao kupata mitaji ya biashara. Alisema kushuka kwa riba ya mikopo kuna maana kwamba idadi ya watu watakaotaka kuwekeza kwenye biashara itaongezeka mara dufu, wakati huo huo wafanyabiashara waliopo watapata fursa ya kupanua biashara zao. “Hii ni dalili njema kwa kuwa uchumi wa nchi utakua zaidi, ajira zitaongezeka na mapato ya wananchi na serikali nayo yataongezeka,” alieleza Profesa Ngowi.

Pamoja na dalili hiyo njema ya kushuka kwa riba ya mikopo, Profesa huyo wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema kuwa jambo hilo linapaswa kwenda sambamba na uboreshaji wa maeneo mengine kama vile miundombinu, nishati ya umeme pamoja na elimu au ujuzi wa wananchi kufanya biashara. Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jehovaness Aikaeli alisema mpango wa kushuka kwa riba ya mikopo ni habari njema kwa wananchi lakini pia kuna mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika hilo.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni uwezo wa mabenki kujiendesha pamoja na kutengeneza faida. Alisema kama kushuka kwa riba za mikopo kutaziwezesha benki kuwa na uwezo wa kujiendesha kama vile kuendelea kuwa na uwezo wa kulipa mishahara na kodi za pango na mambo mengine ya uendeshaji, basi jambo hilo litakuwa zuri kwa pande zote mbili, yaani wananchi na benki pia.

Aliongeza kuwa kushuka kwa riba za mikopo pia kunapaswa kuendane na uwezo wa mabenki kuendelea kutengeneza faida. Alisema kama mambo hayo yatatekelezeka basi kushushwa kwa riba za mikopo kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia sita litakuwa jambo zuri.

Aidha, Mchumi mwingine aliyezungumza na gazeti hili na hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa kama kushushwa kwa riba hiyo kutatokana na sababu nzuri za kiuchumi, basi jambo hilo ni jema kwa kuwa riba ni tatizo kubwa Barani Afrika. Alisema ikilinganishwa na nchi nyingine kama vile za Asia, riba za mikopo kwenye benki Barani Afrika bado ziko juu. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa uchumi, kushushwa kwa riba hizo kutavutia wawekezaji kwenye sekta mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, viwanda lakini pia kutaongeza ajira.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here