SHARE

MOJA ya mambo yanayowaweka watu wengi njia panda ni uamuzi wa kuacha au kuendelea na ajira zao.

Kwa sababu mbalimbali, watu hufikiria kufanya uamuzi wa kauchana na ajira, hivyo kuamua kuandika barua kuwaarifu waajiri wao juu ya jambo hili. kuacha ajira kwa hiari ni haki ya msingi ya mwajiriwa pale anapoona yafaa kufanya hivyo.

Pamoja na ukweli huo, ajira ni moja ya mambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu yeyote yule na upatikanaji wake umekuwa changamoto kutokana na ongezeko kubwa la watafuta ajira huku fursa za ajira zikiwa chache.

Kwa kuzingatia uzito wa sababu hizo, mtu anayetaka kuacha kazi kwa sababu yoyote ile, anatakiwa kufanya tathmini juu ya faida na hasara za uamuzi huo.

Kukurupuka kufanya uamuzi huo bila kujitathmini kunaweza kusababisha majuto na madhara makubwa kwa mtu mwenyewe na jamii inayomzunguka, hasa wategemezi wake.

Je, ni mambo gani ya kuzingatia unapotaka kuacha kazi?

UZITO WA SABABU

Kabla ya kuangalia kitu chochote kile, ni bora kutathmini sababu zinazokufanya kutaka kufanya uamuzi wa kuacha kazi. Wakati mwingine sababu zinazoweza kumfanya mtu akataka kuacha kazi huwa hazina uzito au hukosa mantiki yoyote.

Watu wengine hutumia sababu za muda mfupi kufanya uamuzi ya kudumu. Suala hili si jema kabisa na linahitaji tafakari. Unawaza kuacha kazi kwa sababu tu eti ndani ya ofisi kuna mtu mmoja huelewani naye au una mgogoro naye?

Kuna uwezekano mkubwa wa kutafuta muafaka au usuluhishi ili kurudisha amani itakayofanya kuendelea kufurahia mazingira ya kazi au ajira yako.

Wakati mwingine inahitaji uvumilivu tu, kama wewe na mkuu wako wa idara hampikii chungu kimoja, kumbuka dhamana ya uongozi katika taasisi uwa ni ya muda tu.

Usije kuacha kazi ambayo wakati mwingine unachotakiwa kufanya ni kunyamaza tu na kuendelea na mambo yako.

TATHMINI MBADALA WA KAZI

Kama ajira yako ndiyo njia pekee ya kupata kipato chako na unataka kuacha kazi hiyo, kuna haja ya kujihoji kujua endapo utaacha kazi hiyo ni nini mbadala wake. Si vyema kuamua kuacha kazi kama haujui au huna hata mbadala wa ajira yenyewe ili kupata fedha za kujihudumia na kuhudumia wengine.

Endapo mbadala ni kupata ajira, nyingine hakikisha umeshapata ajira kwingine na kujiridhisha kuwa unakotaka kwenda na bora zaidi ndiyo ufanye mchakato wa kuacha ajira yako.

Wako watu wanaoahidiwa ajira sehemu zingine na kuamua kuacha ajira zao za sasa lakini mwisho wake ahadi hizo zinayeyuka.

Kama mbadala ni biashara au shughuli nyingine yoyote ile hakikisha kuwa shughuli hiyo itakuwa ya uhakika na haitakufanya ujutie uamuzi wako.

Jambo la muhimu kukumbuka ni ukweli kwamba kila eneo la kazi lina changamoto zake, hivyo usije kuacha sehemu yenye unafuu na kwenda sehemu yenye changamoto zaidi.

MADHARA YA KISHERIA

Tunapoajiriwa huwa tunaingia makubaliano ya kisheria kati yetu na waajiri. Makubaliano hayo yana ambatana na maridhiano yaliyopo kwenye mkataba wa ajira.

Ni vyema kupitia na kutathmini madhara kadhaa unayoweza kukabaliana nayo endapo utaacha kazi. Ni wapi ulitumia ajira yako kama dhamana? Kukopa benki?

Ni vyema kujiuliza maswali kadhaa ili kujua vyema ni nini utakumbana nacho baada ya kuacha ajira yako. Usije kuacha ajira ukadhani utapata nafuu ya maisha lakini ndiyo ukawa mwanzo wa migogoro na mwajiri wako au watu wengine.

NAMNA YA KUACHANA NA MWAJIRI WAKO

Kwa sababu yoyote ile inayokufanya uache kazi, kumbuka kuondoka vizuri. Watoto wa mjini wanasema ‘usinyee kambi’.

Wapo watu wanaomua kuacha kazi huku wakiondoka kwa maneno ya dharau, chuki na kejeli. Zingatia matumizi ya lugha ya kistaarabu na kuondoka kiungwana na ukiweza kuandika hata barua ya kushukuru kwa kuitumikia ofisi au mwajiri wako kwa kipindi ulichofanya naye kazi.

Haujui ya kesho, kuna uwezekano ukajikuta unahitaji kurudi ulipotoka, hivyo tengeneza mazingira ya kuondoka bila kinyongo au mgogoro na mtu yeyote katika taasisi yako.

TAFUTA USHAURI

Uamuzi wa kuacha kazi unaweza kuwa ni wako binafsi lakini kutoa uamuzi bila kushirikisha wengine kunaweza kuwa na athari nyingi sana. Wakati mwingine kile unachoona sawa kinaweza kisiwe sawa kwa mtazamo wa watu wengine wanaoweza kukupa ushauri wenye tija.

Kadhalika, uamuzi wa kuacha kazi kwa hiari unaweza kuwa na athari kwa watu wengi wakiwamo wategemezi wako.

Tafuta watu wa karibu unaowaamini na wanaoweza kukupa ushauri wa kujenga kisha washirikishe suala hilo.

Inawezekana unataka kuacha kazi ili uende sehemu nyingine kwenye ujira mnono zaidi lakini kwa kumshirikisha mwajiri wako dhamira yako ya kuacha kazi akaamua kukuboreshea maslahi yako.

UTAYARI NA UWEZO KUISHI BILA AJIRA

Kwa sababu mbalimbali, wako walioamua kuacha ajira zao kwa kufuata mkumbo eti kwa sababu kila mtu anaacha kazi na wao wanaona ni busara kufanya hivyo.

Kila mtu ana sababu zake na anajua njia atakazotumia kuishi baada ya hapo. Tumia busara kujitathmini kuona kama huu ni muda sahihi wa kufanya uamuzi mkubwa kama huu.

Endapo unaona bado nafsi yako inasita kuchukua uamuzi kama huu, ni vyema kujipa muda ili kujua kama kweli huu ni wakati sahihi wa kufanya uamuzi kama huo. Usjie ukaamua kuacha kazi au ajira yako na kisha ukageuka kuwa tegemezi.

Uwezo na utayari kufanya uamuzi kama huu wakati mwingine unachangiwa na maandalizi ya muda mrefu.

Unatakiwa kuandaa mazingira ya kiuchumi na hata kisaikolojia ili umudu maisha baada ya ajira yako ya sasa. Kumbuka mabadiliko yoyote huja na changamoto zake.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, anapakikana kwa 0659 08 18 38, kelvinmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here