SHARE

Yametimia! Baada ya uvumi wa muda mrefu, hatimaye kocha George Lwandamina amejiunga na timu yake ya zamani Zesco United ya Zambia bila ya kuweka wazi mkataba huo ni wa muda gani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Zesco, Richard Mulenda na kuchapishwa katika ukurasa wa Facebook wa klabu hiyo ilisema “Zesco United Football Club (FC) inayofuraha kumtangaza George Lwandamina kuwa Kocha Mkuu mpya wa klabu hii. Lwandamina anachukua nafasi ya kocha Tenant Chembo (TC) aliyetangaza kujiuzulu nafasi hiyo Jumapili Aprili 8,2018.

“Hatuna wasiwasi kuhusu uwezo, tunaamini ataendeleza rekodi yetu ya ushindi na kuendelea kutawala soka la Afrika pamoja na utamaduni wa kushinda mataji likiwa ni lengo letu kuu Zesco United, kuanzia wachezaji hadi mashabiki.”

“Kwa niaba ya uongozi wa klabu hiyo tunampongeza George Lwandamina kwa kuchaguliwa nafasi hiyo, pia tunawashukuru kila mmoja katika klabu yetu,” ilimaliza kusema taarifa hiyo.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa juu ya suala la Lwandamina kusaini mkataba Zesco, alisema hayo ni masuala ya kocha.

“Kama ndiyo iko hivi, tutatafuta kocha mwingine,” Mkwasa alijibu kwa kifupi.

Awali, Mkwasa alisema hana taarifa za Lwandamina kuondoka kwa kuwa bado ana mkataba unaomalizika mwanzoni mwa Juni.

“Kocha bado tupo naye kama ni kuondoka mimi kama mtendaji wa klabu sina taarifa hizo. Mkataba wake utakwisha Juni mwanzoni. Kuhusu ishu ya kumuongezea mkataba ama la, hayo ni masuala binafsi ya klabu na yatajadiliwa na kamati,” alisema Mkwasa.

Pia Mkwasa, ambaye kitaaluma ni kocha, alisema hana taarifa za Yanga kumrejesha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Hans Pluijm anayeinoa Singida United kujaza nafasi ya Lwandamina.

Vyombo vya habari vya Zambia vililiripoti kuwa kocha Lwandamina anakwenda Zesco kuchukua nafasi ya Tenant Chembo “TC” aliyebwaga manyanga kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo.

Taarifa zilizopatikana jana jioni kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Yanga zinadai kuwa Lwandamina ameondoka kutokana na kutoelewana na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo inayohaha kutetea ubingwa.

Chanzo hicho kinadai kuwa kuondoka kwa Lwandamina ni uzembe wa baadhi ya viongozi kushindwa kusimamia mambo muhimu anayotaka kocha huyo.

Mapema jana asubuhi, Lwandamina alimtaka msaidizi wake, Noel Mwandila kumsindikiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa safari ya kurejea Zambia.

Jana mazoezi ya mabingwa hao wa Bara yalisimamiwa na Mwandila, akisaidiana na Shadrack Nsajigwa.

Mmoja wa mabosi wa Yanga ambaye hakutaka jina kutajwa  alisema wanafuatilia kwa karibu suala hilo.

“Mpaka sasa tumechanganyikiwa. Anayetuambia Lwandamina ameondoka naye hajui kipi kimemrudisha kwao, lakini hata sisi wenyewe hakutuaga na sio kawaida yake. Kwa hiyo hatuwezi kuwa na kauli yoyote mpaka tukishazungumza naye,” alisema kigogo huyo.

Lwandamina ana rekodi ya kuifikisha Zesco nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2016 kabla ya kujiunga na Yanga.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here