SHARE

KOCHA Mkuu wa Singida United, Mholanzi, Hans van der Pluijm, anapewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Mromania, Aristica Cioaba katika kikosi cha mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC, imefahamika.

Taarifa kutoka katika klabu ya Azam FC zinasema kuwa klabu hiyo haina mpango wa kumuongeza mkataba mpya Cioaba baada ya msimu huu kushindwa kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA.

Habari zaidi zinaeleza kuwa tayari uongozi wa Azam FC na Pluijm, kocha wa zamani wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wameshafanya mazungumzo ya awali kuhusiana na ofa hiyo.

“Wakati wowote Pluijm anaweza kutangazwa kuwa kocha mpya wa Azam FC , atasaini mkataba na baadaye watatambulisha,” kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo Pluijm, jana alipotafutwa na gazeti hili kuthibitisha kama amefanya mazungumzo na klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam, hakupokea simu.

Azam FC ambayo inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa pointi 45 imetolewa kwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo na vile vile iliyaaga mashindano ya Kombe la FA baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro penalti 9-8 kwenye mechi ya hatua ya robo fainali baada ya sare ya 0-0.

Kwa maana hiyo, Azam FC mwakani haitashiriki tena katika mashindano ya kimataifa.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here