SHARE

RAIS John Magufuli amesema Hayati Edward Sokoine ni shujaa ambaye Watanzania wanapaswa kumuenzi kwa kujenga umoja, kupiga vita rushwa, ufisadi na kuchapa kazi.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Magufuli alisimulia jana mahali na mzingira ya alipopokea taarifa za kifo hicho miaka 34 iliyopita.

“Katika siku kama ya leo Aprili 12, mwaka 1984 nikiwa (kambi ya) Mpwapwa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) nikitumikia jeshi langu, ‘Operesheni Nguvu Kazi’ tukatangaziwa kifo cha marehemu Edward Moringe Sokoine,” aliandika Rais Magufuli.

“Ilikuwa siku ya majonzi shujaa huyu niliyemjua na kumshabikia ikawa siku yake ya mwisho.”

Rais Magufuli aliandika zaidi: “Wakati tunapoadhimisha siku kama hii ya kifo chake, Watanzania tuige mfano wake kwani alikuwa msema kweli, asiyeogopa, mpiga vita rushwa, ufisadi, unyonyaji, mzalendo wa kweli na alichukia rasilimali za Watanzania kuibwa.”Alieleza Sokoine hatasahulika katika historia ya Tanzannia na alitoa wito kwa Watanzania kumuiga na kumuenzi kwa kujenga umoja, kupiga vita rushwa na kuchapa kazi.

SOKOINE NI NANI?Hayati Sokoine alizaliwa Agosti 1, 1938 katika Wilaya ya Maasai Land ambayo kwa sasa inafahamika kama Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari 1958 alijiunga na chama cha Tanu mwaka 1961 na baada ya kushika nyadhifa tofauti mwaka 1977 aliteuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu.

Akiwa Waziri Mkuu, kutokana na uzalendo wake alimuomba Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, aache kazi kwa muda ili aende kusomea zaidi mambo ya ujamaa nchi za nje.

Hii ilikuwa kati ya mwaka 1981 hadi mwaka 1983 aliporejea nchini kuendelea na nafasi yake.

Ilipofika Aprili 12, mwaka 1984, Sokoine alipata ajali mbaya ya kugongwa na gari eneo la Wami Dakawa, kwa sasa Wami Sokoine, mkoani Morogoro na kufa papo hapo.

Gari hilo lililomgonga lililokuwa likiendeshwa na mkimbizi wa kisiasa kutoka Afrika Kusini, Dumisani Dube.Marehemu Sokoine atakumbukwa kwa misimamo na mitazamo yake ambayo aliamini katika siasa za ujamaa zaidi, haki, usawa na uwajibikaji.

Pia alichukia vitendo vya rushwa, hujuma, uhujumu uchumi, ulanguzi na magendo ambavyo serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli inapiga vita vikali dhidi yake.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here