SHARE

LICHA ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyofanyika juzi dhidi ya Mbeya City, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pierre Lechantre, hakufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mchezo huo.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika, Lechantre, alisema kuwa amefurahi kupata pointi tatu na kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa, lakini wachezaji wake walishindwa kufuata maelekezo aliyowapa kuelekea mchezo huo.

Lechantre alisema kuwa hali hiyo ni hatari hasa pale inapotokea wakati timu yako ikiwa haijafunga bao lolote na mpinzani anapofanikiwa “kukubana” na kumiliki mpira na kusababisha kukosa ushindi.

“Sijafurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wangu, hawakufuata vyema maelekezo niliyotoa katika mechi hii (dhidi ya Mbeya City), waliwaruhusu kutawala na kuwazuia kuonyesha aina ya mfumo nilioupanga,” alisema kocha huyo raia wa Ufaransa ambaye anasaidiwa na Masoud Djuma, kutoka Burundi.

Naye mshambuliaji kinara katika ligi hiyo, Emmanuel Okwi, alisema kuwa bado mbio zao za kuwania ubingwa zinaendelea kwa sababu pointi nane walizoachana na Yanga ni chache.

“Lengo langu kwanza ni kuisaidia timu, na siwezi kuzungumzia ubingwa kwa sababu Yanga tumewapita pointi nane lakini wao wanamechi mkononi, tunahitaji kupambana ili kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema Mganda huyo.

Kikosi cha Simba kinatarajia kuendelea na mazoezi leo kwa ajili ya kujiandaa kuwakaribisha Tanzania Prisons katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayofanyika Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini huku ikiwa na kumbukumbu ya kuwafunga “Maafande” hao katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Simba ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa inaongoza ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Mei 26 mwaka huu ikiwa na pointi 55 ikifuatiwa na mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 47, kabla ya matokeo ya jana wakati Azam FC ilipotarajiwa kuivaa Ruvu Shootingi kwenye Uwanja wa Mlandizi,Pwani.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here