SHARE

SHIRIKA la Kutetea Haki za Binadamu Duniani (Amnesty International), limesema idadi ya watu waliohukumiwa adhabu ya kifo, imepungua mwaka uliopita ikilinganishwa na miezi 12 iliyopita.

Katika ripoti yake mpya imesema karibu watu 1,000 walinyongwa mwaka 2017, huku asilimia 84 ya watu hao adhabu yake ikitekelezwa katika nchi za Iran, Saudi Arabia, Irak na Pakistan.

Aidha, nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, zimetajwa kupiga hatua katika harakati za kupinga adhabu ya kifo na nchi 20 za Afrika zimeshafuta adhabu hiyo.

Inatoa mfano wa taifa la Guinea, kwamba limeshafuta adhabu ya kifo kwa uhalifu wowote ule, huku Kenya ikiwa na msimamo kuwa adhabu ya kifo si ya lazima, licha ya kwamba bado inayo hukumu hiyo.

Burkina Faso, pia imesifiwa kwa muswada wake wa katiba unaohusisha kipengele cha kuondoa adhabu ya kifo na sheria mpya ya Chad inaruhusu kutekelezwa hukumu hiyo, pale mtuhumiwa atakapobainika kuwa na hatia ya ugaidi.

”Watu wengi wanaounga mkono adhabu ya kifo, wanasema adhabu ya kifo ikiwepo itasaidia watu hawatatenda uhalifu, lakini utafiti uliofanyika duniani kote unaonyesha kuwa hilo haisaidii,” anasema Seif Magango, Ofisa wa Amnesty International, Kanda ya Afrika Mashariki.

”Tunaikemea adhabu ya kifo ambayo tunaiona ni ya kinyama, kwa sababu katika nchi kama Marekani, adhabu hizi zinapotekelezwa unabaini kuwa uchunguzi wa vinasaba unapofanywa inakuja kugundulika kuwa wakati mwingine aliyehukumiwa si aliyefanya makosa,” anasema Magango.

Licha ya kwamba nchi 20 barani Afrika zimefuta hukumu ya kifo kwa makosa yote, Somalia na Sudan Kusini zimesalia kuwa nchi pekee zinazoendeleza hukumu hiyo hadi mwaka jana, ikilinganishwa na mwaka 2016, nchi tano zilikuwa zinatekeleza hukumu hiyo.

UTEKELEZAJI HUKUMU

Somalia: Huko kuna sheria zinazoidhinisha njia za kifo, hasa kwa washukiwa wa uhalifu. Kuna badaji ya matukio ambayo hukumu ya kifo ilitekelezwa na Mahakama ya Kijeshi, dhidi ya watu 12 wa mashambulizi mwaka 2017.

Pia, kabla ya hukumu hiyo, mwezi April mwaka huo, watuhumiwa 11 waliripotiwa na vyombo vya habari kuwa walinyongwa, hali kadhalika jimboni Puntland lilitekeleza hukumu ya kifo kwa wafungwa 12 mwaka huo.

Takwimu za Umoja wa Mataifa, zinaonyesha takriban hukumu za vifo 64 zilitolewa mwaka 2016 nchini Somalia.

Sudan: Sheria ya Sudan Kusini ya mwaka 2008 ya uhalifu ya kabla ya uhuru wa taifa hilo bado inatekelezwa ikielezea kuwa hukumu ya kifo itatekelezwa kwa kunyongwa.

Hata hivyo hukumu hiyo imekuwa ikitekelezwa na serikali pamoja na makundi ya uasi dhidi ya wapinzani wao.

Tanzania: Amensty International inasifu uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli aliyewasamehe, watuhumiwa wa kunyongwa 61, sambamba na wengine wa makosa mbalimbali 1,821.

Pia, wafungwa wengine 8,157 wamepunguziwa adhabu zao, inadaiwa idadi hiyo ya msamaha kwa wafungwa ni rekodi kubwa zaidi, ikijumuisha waliofungwa wa maisha.

Saudi Arabia: Mahakama moja nchini Saudi Arabia, imewapa hukumu ya kifo watu 15 wakidaiwa ujasusi, wametuhumiwa kwa mtandao wa ujasusi wa kimataifa na kutoa taarifa muhimu za kijeshi.

Marekani: Majimbo mengi nchini Marekani yalitumia uchaguzi mkuu, kama fursa ya kuweka kwenye mzani maswali kwa umma kuhusu masuala kama ushuru, kima cha chini cha mshahara na hukumu ya kifo.

Huko jimbo la Nebraska, kuliidhinisha kwa mara nyingine hukumu ya kifo, ingawa jimbo hilo halijawahi kutekeleza hukumu yake kwa mfungwa yeyote tangu mwaka 1997, likiwa na jumla ya watu 10 walioorodheshwa wakato huo wa uchaguzi.

Katika jimbo la Colorado, waliidhinisha kifo cha kusaidiwa kwa wagonjwa mahututi kupitia dawa ambayo mtu anaweza kujichagulia mwenyewe.

MNIGERIA ALIYEHUKUMIWA SINGAPORE

Mwaka 2016, Singapore lilikataa ombi la msamaha kutoka kwa raia wa Nigeria, aliyepangiwa kunyongwa kwa kupatikana na bangi, shirika la haki za kibinadamu la Amnesty International liliripoti.

Familia ya Chijoke Stephen Obioha, ilifahamishwa kuhusu hatua hiyo. Mtuhumiwa huyo, alikutwa kilo 2.6 za bangi Aprili 2007, kiasi kilichozidi kipimo cha gramu 500, ambacho humfanya mtu kuhukumiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya, kwa mujibu wa sheria za Singapore.

Ofisa wa Amnesty International, Rafendi Djamin, alisema shirika hilo lilishangazwa na hatua hiyo ya Singapore kumnyima mshtakiwa huyo msamaha.

Alisema shirika hilo lina matumaini kwamba Singapore isingetekeleza adhabu hiyo “katili na isiyoweza kubatilishwa dhidi ya mtu huyo aliyehukumiwa kifo kwa kosa ambalo halifai adhabu ya kifo.”

“Hukumu ya kifo si suluhu. Haitaangamiza dawa zote za kulevya Singapore. Kwa kuwanyonga watu kwa makosa ya kuwa na dawa za kulevya, ambayo hayafikii kiwango cha makosa makubwa ya uhalifu, Singapore inakiuka sheria za kimataifa. “Mataifa mengi ulimwenguni yameacha adhabu hii ya kikatili, kinyama na ya kudunisha.”

Wakati Singapore inatoa hukumu ya kunyongwa kwa kosa la kupatikana na bangi, California imeidhinisha matumizi ya bangi kujifurahisha. Hii ni taarifa ya Novemba 2016.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here