SHARE

ACHANA na pacha zote unazozijua kwenye Ligi Kuu za Ulaya ikiwemo ile ya Sadio Mane na Mohamed Salah ya Liverpool, hapa Bongo kuna pacha moja tu matata kwenye Ligi Kuu Bara.

Pacha hiyo ni ya Emmanuel Okwi na John Bocco kwenye kikosi cha Simba tena hii ya Mfaransa, Pierre Lechantre ambayo ni moto kwelikweli na haijapata kutokea. Bocco na Okwi kwa pamoja wamepasia nyavuni mara 31 msimu huu, lakini habari njema ni kuwa, kila mmoja anafurahi kucheza pembeni ya mwenzake.

Okwi, ambaye amekuwa shujaa wa Simba kila anapopata nafasi ya kuichezea, amesema hakuna kitu kinachompa mzuka kama kucheza na Bocco.

Amesema Bocco anajua kupasia nyavuni, kumiliki mpira na kumlisha pasi za mwisho za maana hivyo, kama wataendelea hivi kwa misimu kadhaa basi mabeki watakuwa na kazi ya kuokota mipira nyavuni tu.

“Bocco ana uwezo wa kufunga na kunitengenezea nafasi nyingi za mabao ambazo kazi yangu ni kupasia nyavuni tu. Tumekuwa na maelewano mazuri katika kucheza na kama tukiendelea kuwa pamoja naona tutafunga magoli mengi zaidi muda wote,” alisema.

“Nilikuwa namfahamu Bocco tangu akiwa Azam na nilipoanza msimu tukiwa pamoja nilijua tu tutakuwa na mabao mengi ya kufunga na tunataka kufunga magoli mengi zaidi ya sasa ili tuwe wafungaji bora wa muda wote Simba.

“Tuna kikosi imara na nawapongeza wachezaji wenzangu kwani, wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi za kufunga na ushirikiano huo umechangia kufukia idadi ya magoli haya ambayo tumefunga,” alisema Okwi, ambaye aliongezea hata mfumo wao umetengenezwa kuwazunguka wawili hao kufunga tu.

Kocha wa Simba Mfaransa Pierre Lechantre alisema anavutiwa na viwango vya Bocco na Okwi na uwezo wao wa kufunga na anajivunia kikosi chake kuwa na mastraika hao ambao ni hatari katika ligi.

Alisema kila kocha anafurahi kuwa na wachezaji wanaofanya vizuri kikosini na kwamba, anaridhishwa na maendeleo na njaa njaa ya mafanikio uwanjani.

“Kazi ya kufunga ambayo wanaifanya Bocco na Okwi inanipa faraja na wanafanya kazi ya kuturahisishia kupata ushindi kila mechi kwani, licha ya kucheza vizuri ushindi ndio unatakiwa wanafanya hivyo kwa ufasaha,” alisema Lechantre.

Beki wa kushoto wa Simba Asante Kwasi na winga Shiza Kichuya nao hawapo nyuma katika kutupia kwani mpaka sasa wamefunga magoli saba kila mmoja.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here