SHARE

KAMPUNI ya Ubia ya StarMedia imekubali hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na mapendekezo yake na wakati zikifanyiwa kazi, imeamua kutoa Sh bilioni tatu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kama ruzuku kwa mwaka huu.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitoa taarifa hiyo jana mjini hapa kupitia tamko lake kwa waandishi wa habari kuhusu hoja zilizoibuliwa na CAG kuhusu kampuni hiyo Hoja za CAG Chini ya utaratibu ambao serikali imejiwekea; wa wizara kujibu hoja mbalimbali zilizoainishwa katika ripoti ya CAG, Dk Mwakyembe amesema wameanza vizuri na wanaamini changamoto zote zilizoanishwa na CAG zitarekebishwa haraka na umma utakuwa ukiarifiwa.

Alieleza yaliyobainishwa na mdhibiti na mkaguzi pamoja na kamati ya majadiliano aliyoiunda kuwa ni, upungufu wa utendaji na uendeshaji wa kampuni.

Miongoni mwa sababu zilizochangia upungufu ni mkataba mbovu wa ubia uliompa mbia Star Communication mamlaka makubwa ya usimamizi wa fedha na uendeshaji bila kumshirikisha mbia TBC mwenye asilimia 35 ya hisa zote.

Sababu nyingine ni bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya ubia kukosa sauti na mamlaka katika uendeshaji wa kampuni ya ubia na badala ya uamuzi mwingi kufanywa na Star Communication. Nyingine ni taarifa za fedha na uendeshaji kufuata mifumo na taratibu na lugha za Kichina hivyo kumwacha TBC kuwa kama mtazamaji asiye na picha kamili kuhusu taarifa za fedha na uendeshaji.

“Hata CAG hakuweza kuingia kwenye mfumo huo kukagua mwenendo wa mapato ya kampuni wakati wa kufanya ukaguzi maalumu,” alisema Dk Mwakyembe. Dk Mwakyembe alitaja sababu nyingine ni udhaifu katika uamuzi wa wawakilishi wa serikali kwenye kampuni ya ubia ya StarMedia ambao ulijitokeza mwaka 2014.

Udhaifu ulitokana na Mkurugenzi Mkuu wa TBC aliyepita ambaye wakati huo huo alikuwa mwenyekiti wa bodi kugomea kusaini hesabu za kampuni za mwaka 2014 kwa hoja kuwa baadhi zilikosa uthibitisho na tangu hapo, akajiuzulu uenyekiti na kuwaachia Wachina kuongoza kampuni.

Waziri alisema CAG alibaini pia maeneo makubwa matatu ambayo StarMedia ilikuwa na upungufu nayo ni: vifaa vya Sh bilioni 34.4 venye msamaha wa kodi kutotumika kwenye mradi kusudiwa; kanuni ya StarMedia kutoza uchakavu wa dola za Marekani milioni 30.11 isivyo halali na kamuni kutochangia gharama ya mtaji dola za Marekani 650,000.

StarTimes yasalimu “Baada ya majadiliano ya muda mrefu na wenzetu wa StarTimes Group, wenzetu hatimaye waliikubali taarifa ya CAG na mapendekezo yake yote,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa ilimbidi na yeye kushiriki majadiliano ili kuyaharakisha yafikie mwisho.

Alitaja yaliyokubaliwa na kampuni hiyo ni pamoja na kuipa mara moja Bodi ya Wakurugenzi madaraka yake stahili na hivyo kuruhusu uwazi wa kutosha katika uendeshaji wa kampuni. Mengine ni kuruhusu TBC na wataalamu wake kuingia kwenye mifumo ya Tehama na uendeshaji na kuleta uwiano upande wa wafanyakazi na viongozi wa kampuni hiyo ya pamoja.

“Aidha, wakati hoja nyingine zikifanyiwa kazi, Kampuni ya StarMedia itatoa kiasi cha shilingi bilioni tatu kwa TBC kama ruzuku mwaka huu 2018,” alisema Dk Mwakyembe.

Wakati huo huo, Dk Mwakyembe ameagiza Bodi ya TBC na Mwenyekiti wa Bodi ya StarMedia Tanzania kusimamia kwa karibu na kikamilifu utekelezaji wa hoja zote zilizopo kwenye mkataba huo.

Wizara ilivyoingilia kati Dk Mwakyembe ambaye amemshukuru CAG, Profesa Mussa Assad na wataalamu wake kwa kazi nzuri waliyoifanya ya ukaguzi maalumu kuhusu uendeshaji wa kampuni hiyo ya ubia, alisema Septemba 2016 serikali kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya TBC ilimwomba CAG afanye ukaguzi maalumu wa StarMedia kwa kushindwa kutoa gawio kwa wabia wake kwa miaka saba mfululizo.

Mei 20, mwaka jana, Rais John Magufuli alipofanya ziara katika ofisi za TBC Mikocheni, Dar es Salaam alionesha kutoridhishwa na utendaji wa StarMedia na kuagiza gawio kwa wabia lianze kutolewa.

“Kutokana na agizo la Rais, nilichukua hatua mbili wakati huo huo ukaguzi maalumu wa CAG ukiendelea,” alisema na kutaja hatua hizo ni pamoja na kumuita Rais wa StarTimes Group ambayo ni kampuni mama ya Star Communication ili wajadiliane kuhusu changamoto zinazokabili kampuni na utatuzi wake.

Waziri pia aliunda kamati ndogo chini ya Mkurugenzi wa Habari-MAELEZO, Dk Hassan Abbasi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kiini cha udhaifu katika utendaji wa kampuni.

Novemba mwaka jana, taarifa zote mbili za CAG na kamati ndogo ya Dk Abbasi zilikamilika na kuwasilishwa kwa waziri na yeye aliunda kamati ya majadiliano kati ya serikali na wawakilishi wa StarTimes Group ili kuchambua hoja zilizobainishwa na kuandaa mapendekezo ya namna bora ya kutatua hoja zilizojitokeza.

Februari 20 mwaka huu ndipo kamati ya majadiliano ilipowasilisha kwa waziri taarifa iliyoanisha upungufu wa utendaji na uendeshaji wa kampuni.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here