SHARE

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema itawapanga upya madaktari bingwa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya kila Hospitali ya Mkoa, Kanda Maalum na taifa.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Faustine Ndugulile alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Azza Hamad.

alitaka kujua lini serikali itapeleka madaktari bingwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kutokana na kukabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa.

Akijibu, Dk. Ndugulile alisema, lengo la upangaji huo ni kila hospitali kuwa na madaktari bingwa ikiwamo Hospitali ya Shinyanga.

Alisema hatua hiyo imetokana na uamuzi wa serikali wa kuzihamishia hospitali za rufani za mikoa kuwa chini ya wizara hiyo.

Alisema wizara inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya kina kujua hali halisi ya madaktari bingwa na fani zao katika hospitali zote.

“Baada ya kukamilisha tathmini hiyo, wizara itawapanga upya madaktari bingwa kwa uwiano na mahitaji ya kila hospitali,” alisema.

Alisema ili kuwezesha kutoa huduma za kibingwa, Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, inahitaji kuwa na madaktari bingwa wa fani sita.

Alitaja fani hizo kuwa daktari bingwa wa kinamama na wajawazito, afya ya kinywa na meno, magonjwa ya ndani, mionzi, upasuaji na watoto.

Aidha, alisema wizara inatambua kuwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga kwa sasa ina madaktari bingwa watatu tu.

“Madaktari hawa ni magonjwa ya kinamama na wajawazito, upasuaji na watoto,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here