SHARE

POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam, inamshikilia Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya baada ya kuripoti kituoni hapo na viongozi wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kama walivyoamriwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hatua ya Bulaya kutiwa mbaroni inatokana na kutowapo wakati viongozi wengine wa chama hicho walipojisalimisha polisi.

Viongozi wengine waliotii amri hiyo jana ni pamoja na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Akizungumza na gazeti la Nipashe mara baada ya kutoka kituoni hapo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mwalimu alisema waliripoti jana kama walivyotakiwa wakati mwenzao Bulaya akiendelea kushikiliwa kwa taratibu za ziada.

“Baada ya kuripoti kama Mahakama ya Kisutu ilivyotutaka ikiwa ni sharti la dhamana, mwenzetu Bulaya alipofika kituoni hapo, polisi walimshikilia, hatuna uhakika kama watakaa naye kwa muda gani au wataamua kumshikilia hadi Jumatatu ili wakamuunganishe na kesi yetu,” alisema.

Alisema kulingana na sharti la dhamana lililotolewa kwao, wanawajibika kila Ijumaa kuripoti kituoni hapo na wamekuwa wakisaini na kuondoka.

Katibu Mkuu, Mashinji alisema watakwenda tena mahakamani Jumatatu kuendelea na kesi inayowakabili.

“Tumeambiwa tutaongezewa Esther Bulaya, katika shauri la kesi yetu na polisi wanamshikilia kwa sasa kwa taratibu za kiupelelezi,” alisema.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alipoulizwa kuhusu kushikiliwa kwa Bulaya na kama atapatiwa dhamana, alijibu kwa kifupi, “sifahamu kama yupo hapa”.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here