SHARE

SIKU chache baada ya kuibuka mijadala kuhusu mwanamke aliyezaa na raia wa China na kumtelekezea mtoto, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameweka wazi hatua ya ofisi yake kwamba suala hilo ameliwasilisha kwenye ubalozi wa nchi hiyo umsaidie kufuatilia.

Hatua hiyo inakuja baada ya kuripotiwa tukio hilo lililoibua mijadala katika jamii nchini, ambayo pia imesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii tangu Jumatatu iliyopita.

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) jana, kuhusu tathimini ya wawanake waliotelekezwa na kujitokeza kupata msaada wa kisheria ofisini kwake, Makonda alisema amewasiliana na Ubalozi wa China nchini ambao umeahidi kuwasiliana na kampuni anayofanyia kazi baba wa mtoto huyo.

Makonda alisema ubalozi huo pia umeahidi kumsaidia mtoto huyo ili kupata matunzo watakapombaini baba yake.

“Baada ya kupokea malalamiko ya mama aliyezaa na raia wa China, niliwasiliana na Ubalozi wa China nchini ambao walinipa ushirikiano na kuahidi kuwasiliana na kampuni anayofanyia kazi mwanamume aliyetajwa,” alisema Makonda.

Alisema pia wako wanawake waliojitokeza na kutaja baba wa watoto ambao ni raia wa Msumbiji, Zambia na Oman, ambao ni wengi zaidi.

Makonda alisema wanaume wote kutoka nchi zingine ambao wametajwa, tayari ofisi yake imeshafanya mawasiliano na balozi zake zilizopo nchini na kuwapa taarifa ili kusaidia kupatikana.

“Tumewasiliana na hizo balozi kwa sababu taarifa za hao watu zipo na wale ambao balozi zao hazipo nchini tunashirikiana na wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili kuwapata watu hawa walioamua kukwepa majukumu yao,” alisema.

Wataokaidi kukiona

Alisema wanaume wote waliopewa barua za wito kufika katika ofisi zake kuanzia kesho na wakakaidi watakuwa wamefanya kosa kwa mujibu wa sheria za mamlaka husika.

Alisema kuitwa na kuitikia ni jambo moja, lakini pia kukaidi agizo ni kosa la kuidharau mamlaka iliyopo kisheria.

“Ukiitwa unatakiwa kuja kusikiliza wito, lakini endapo utakaidi agizo, ni kosa lingine la kisheria la kudharau mamlaka niliyonayo.

Na mimi nitakuchukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa mamlaka niliyo nayo kwa sababu kama ninaweza kukufukuza kwenye mkoa wangu endapo nitaona unahatarisha usalama, sembuse hili la kutelekeza mtoto kinyume cha sheria ya mtoto ya mwaka 2009,” alisisitiza Makonda.

Tathimini ya siku tano

Watu waliofika katika siku tano za mwazo alisema ni takribani 5,000 huku waliopewa barua za wito wakiwa 2,400 na wanaume 295, wamekubali kutunza watoto.

Kadhalika alisema idadi ya wanaume waliokubali kupimwa vinasaba (DNA), katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefikia 29.

“Haya ni mafanikio kwa sababu tumeweza kuwasaidia wanawake ambao walitelekezewa watoto na kati ya 5,000 tuliyowasikiliza wanaume 295 wamekutana na maofisa wetu wa Ustawi Jamii na wale wa Dawati la Jinsia kutoka polisi na kukubali kutunza familia zao,” alisema Makonda.

Aliwapongeza wanawake ambao kwa moyo wao waliamua kujitokeza kwa ajili ya kupata msaada huo wa kisheria bila kuhofia jamii itazungumza nini juu yao.

“Hawa kwangu nawaona kama wanawake mashujaa kwa sababu waliamua litakalokuwa na liwe. Na fursa muhimu waliyoipata baada ya kusuluhishwa na wenza waliozaa nao, malipo ya matunzo yatatolewa serikalini na mama atayafuata ofisi ya ustawi wa jamii, hivyo wana uhakika wa kupata fedha za matunzo,” alisisitiza.

Msingi wa kuita wanawake

Makonda alisema msingi wa kuanzisha utoaji msaada wa kisheria ni baada ya kupokea idadi kubwa ya wanawake waliokuwa wakifika katika ofisi hizo kuomba msaada baada ya kuachwa na waume zao.

Alisema pia ongezeko la watoto wa mitaani wanao omba, wengi wao wana wazazi, lakini wamewatelekeza.

Kuhusu aliyoyabaini katika siku hizo tano, alisema wapo wanawake ambao walimua kukimbia kwenye ndoa zao kwa sababu wanaume walitaka kuwatoa watoto kafara ili wapate mali.

“Yapo mambo mengi niliyoyabaini baada ya kukutana na wanawake hawa, lakini kubwa lililoniumiza ni wanawake ambao walikimbia kwenye ndoa zao baada ya wanaume kutaka kuwatoa watoto wao kafara,” alisema Makonda.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here