SHARE

Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita kimelaani mauaji ya wanawake wanne waliouawa April 5, 2018 kwa kunyongwa kwa siku moja kisha miili yao kutupwa porini katika vijiji vya Mimbili na Busengwa wilayani humo.

Miongoni mwa waliouawa wawili ni wa familia moja na wengine wawili ni wa kijiji kimoja ambapo uchunguzi umebaini wawili kati yao walikuwa wajawazito na wote walinyong’wa kwa kutumia kanga walizokuwa wamevaa.

Wakizungumza , wakati wa maadhimisho ya miaka 63 ya Jumuiya ya Wazazi wa CCM iliyofanyika kimkoa wilayani Nyang’hwale, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho, Sofia Bakari alisema tukio la kuuawa wanawake wanne ni la kinyama na linawatia hofu wanawake wote .

Bakari alisema mauaji hayo yanahusishwa na ushirikina na kuiomba serikali na vyombo vya ulinzi kuchunguza tukio hilo ambalo si la kawaida katika mkoa huo.

“Tumekuwa tukisikia na kuona vifo vya vikongwe vikiuawa lakini haya yanatisha wanawake waliouawa wanaumri mdogo mbaya zaidi wawili walikuwa wajawazito kwa mauaji haya na sisi tutaisha sasa, maana hatujui nani muauji hadi sasa,” alisema Sofia
Mbunge wa jimbo hilo,

Hussen Nassoro alisema matukio hayo yamemfanya ashindwe kuhudhuria vikao vya Bunge la bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma na kusema mauaji hayo yanasikitisha na hayavumiliki.

Alisema wilaya ya Nyang’hwale sio salama na kuomba kurudishwa kwa sungusungu waliokuwa wanaimarisha ulinzi vijijini

“Wanawake waliouawa ni wadogo sana mmoja alikua na miaka 18 na mwingine 20 na hata hao wawili wengine hawajafikisha miaka 30 kama tunasema vikongwe ndio wanauawa kwa imani za kishirikina vipi hawa ni nini kimetokea, hii inaleta hofu kubwa” alisema Nassoro.

Wanawake hao waliuawa April 5 na miili yao kugundulika April 7 na taarifa zinasema walikuwa wameenda shambani kuvuna mazao kwa ajili ya chakula na hawakurudi kwenye familia zao hadi miili yao ilipokutwa kwenye pori la Bulolwa baada ya kijiji kuitisha msako wa kuwatafuta

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amewataka wananchi kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli zao kwa kuwa jeshi hilo limeimarisha ulinzi na linaendelea na msako wa kuwasaka wauaji hao.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here