SHARE

MASHABIKI wa Simba wanacheeka baada ya kuona moshi unafuka huko mtaa wa pili huku wenyewe wakiendeleza ushindi. Lakini, kocha wao Mfaransa Pierre Lechantre amezisikia tambo za mashabiki wao na kuwapasha kwamba, Simba anayotaka bado hajaipata na kuwa ikikamilika mbona wapinzani watajuta.

Hata hivyo, Lechantre alisema pamoja na kutoridhishwa na soka inalocheza kikosi chake kwa sasa, faraja yake kubwa ni kuona msimamo unasomeka wakiwa kileleni tena kwa pointi nane dhidi ya Yanga.

Kwa sasa Simba ina pointi 55 na mabao 55 katika mechi 23 ilizocheza mpaka sasa huku ikiwaacha mbali wapinzani wao, Yanga yenye pointi 47 walizovuna kwenye mechi 22.

“Nina viwango vyangu ninapofundisha soka, ambavyo napenda kikosi changu kicheze uwanjani, Simba bado haijafika hivyo ninaendelea kuleta vitu vipya ili kupata kikosi ambacho ni kipana na kinachocheza soka la kiwango cha juu. Japo naridhika na matokeo uwanjani kwani, tunapambana kupata ushindi, lakini naseme tu siku Simba ikikamilika basi hakuna Yanga wala timu itakayotia mguu kuikabili Simba. Kuna wakati tunacheza taratibu na napenda tucheze kwa kasi kushoto na kulia, hii ni aina ya mashambulizi ambayo mpinzani anabaki amezubaa tu, lakini wao bado wanacheza taratibu,” alisema kocha huyo ambaye huenda vijana wake watakuwa wamechoka kutokana na mechi mfululizo.

Lechantre amesema kwa sasa kikosi chake kinatumia mfumo wa 3-5-2 ambao unampa fursa kucheza soka la kushambuliza zaidi, japo anawatumia washambuliaji wawili mbele.

Lipuli hofu tupu

Kama unadhani huo moto wa Simba unazikosesha usingizi timu kubwa kama Yanga na Azam pekee, basi utakuwa umekosea sana kwani huko Lipuli ni presha tupu unaambiwa.

Kocha wa Lipuli FC, Amri Said alisema Simba inasumbua na wana kiu ya ubingwa hivyo, atatumia muda kuisoma vizuri kwenye mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons. Simba na Prisons zitakutana Aprili 20 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na Said amesema atatumia mchezo huo kuwasoma Simba.

“Simba moto wake sio wa kitoto, wanataka ubingwa msimu huu, hivyo tunahitaji kuwasoma vizuri kwenye mchezo dhidi ya Prisons ili tujue wapi kwa kuwabana. Mechi ya kwanza tulitoka sare kwa bao la Asante Kwasi, ambaye wamemchukua tayari,” alisema na kuongeza:

“Ukikutana na timu inayotaka ubingwa ama kushuka daraja ni lazima ujipange kwelikweli.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here