SHARE

MTOTO amezaliwa nchini China kupitia kwa mwanamke aliyebeba ujauzito, miaka minne baada ya wazazi wa mtoto kufariki katika ajali ya gari, vyombo vya habari China vinaripoti.

Wazazi hao waliofariki mnamo mwaka 2013, walitoa mayai kadhaa yaliyogandishwa kwa matumaini kwamba watazaa kupitia mfumo wa IVF.

Baada ya ajali, wazazi wao waliwasilisha shauri mahakamani wakitaka kuruhusiwa kuyatumia mayai hayo.

Mtoto huyo mchanga wa kiume alizaliwa Desemba mwaka uliopita kupitia kwa mwanamke aliyebeba mimba huko Laos na kisa hicho kiliripotiwa kwa mara ya kwanza wiki hii na gazeti la The Beijing News.

Gazeti hilo limeeleza jinsi hakujawahi kushuhudiwa kesi ya aina hiyo na ndio sababu iliyowalazimu wazee wa wazazi wa mtoto huyo kuwasilisha shauri mahakamani kabla ya kuanza mpango wa kutafuta mbebaji mimba hiyo.

NI KISA CHA KWANZA

Wakati wa ajali hiyo, mayai yalikuwa yamehifadhiwa vizuri katika hospitali huko Nanjing na yalikuwa yamegandishwa katika nyuzi joto chini ya 196 katika tanki lililojaa gesi ya maji ya Natrojeni.

Mahakama iliwaruhusu bibi na babu wa mtoto huyo kumiliki mayai hayo yaliyogandishwa.

Hakukuwepo na kesi ya aina hiyo awali kuweza kusaidia kujua iwapo wanaweza kurithi mayai ya watoto wao, kwa mujibu wa ripoti.

Hatimaye waliruhusiwa kuyatumia mayai hayo, lakini tatizo jingine likazuka. Mayai hayo yangeweza kutolewa katika hospitali ya Nanjing iwapo tu kungekuwa na uthibitisho kuwa hospitali nyingine iko tayari kuyahifadhi.

Lakini kutokana na wasiwasi wa kisheria kuhusu mayai ambayo hayajapandikizwa, ilikuwa ni vigumu kupata taasisi nyingine ya afya nchini China iliyotaka kujihusisha.

Na kutokana na kwamba ubebaji mimba ya mtu mwingine ni haramu China, nafasi iliyosalia ilikuwa ni kutafuta mbebaji mimba katika nchi za nje.

KUTHIBITISHA UZAZI NA URAIA

Hatimaye, babu na bibi yake mtoto huyo walishirikiana na shirika linalotafuta wanawake wanaobeba mimba za watu wengine na waliangukia eneo la Laos, ambako mpango huo unaruhusiwa kisheria.

Kwa sababu hakuna ndege inayobeba gesi ya natrojeni kwa kiwango cha kujaa chupa ya chai, mzigo huo adimu ulisafirishwa kwa gari.

Na huko Laos, mayai yalipandikizwa ndani ya kizazi cha mama mbebaji na ilipofika Desemba 2017 mtoto huyo wa kivulana alizaliwa.

Uraia wa mtoto huyo, aliyepewa jina Tiantian, lilikuwa ni tatizo jingine na kwa hivyo waliamua azaliwe China na sio Laos, ambapo ilibidi mwanamke huyo asafirishwe kwa viza ya kitalii.

Bibi na Babu ya mtoto huyo wanasema wamefurahi sana kwamba kizazi chao sasa kitaendelea.

BBC


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here