SHARE

SERIKALI imeokoa dola za Marekani bilioni 10.25 (zaidi ya Sh trilioni 20) kuanzia Julai mwaka 2004 mpaka Desemba mwaka jana kutokana na matumizi ya gesi asilia.

Katika kipindi hicho fursa mbalimbali zimepatikana kutokana na nchi kuwa na gesi hiyo kama kampuni za ujenzi, ajira, uboreshaji wa bandari, fursa kwa kampuni za ulinzi uanzishwaji wa vyuo vya mafunzo na mengineyo.

Mtafiti wa Mkondo wa Chini wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Aristides Kato aliyasema hayo wakati wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyoandaliwa na shirika hilo kwa lengo la kueleza mikakati yake kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Alisema mpaka sasa asilimia 50 ya uzalishaji wa umeme nchini unatumia gesi asilia huku kukiwa na viwanda 37 vinavyotumia gesi hiyo na taasisi tatu, hatua iliyowezesha kuokoa mabilioni hayo ya fedha katika kuagiza nishati hiyo kutoka nje ya nchi.

Alisema katika bomba kuu la gesi asilia kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam wameishaanza kupata wateja na tayari wamekiunganisha kiwanda cha vigae cha Goodwill kilichopo eneo la Mkuranga kinachotumia futi za ujazo milioni tano za gesi kwa siku lakini pia kuna viwanda vingi katika eneo hilo, na Bagamoyo wanafanya nao mazungumzo na wamefikia katika hatua nzuri kwa ajili ya kuanza mradi.

Alisema mpaka sasa licha ya kuwepo kwa gesi nyingi ya futi za ujazo milioni 350 matumizi ya Tanesco na kiwanda cha vigae ni asilimia 26 huku wakitumia asilimia 11 tu ya uwezo wa bomba la gesi kusafirisha.

Pia alizungumzia kiwanda cha kuzalisha mbolea kuwa mazungumzo yanaendelea na changamoto ni katika bei ya gesi na tayari kikosi kimeundwa kutoka taasisi mbalimbali kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo huku tayari kampuni ya kuendesha kiwanda hicho ya Tanzania Mbolea and Petrochemical Company (TAMPCO) ikiwa tayari imesajiliwa na kuongeza kuwa kiwanda hicho kitatoa ajira 3,500 kwa Watanzania.

Mhandisi wa Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO) ambayo ni kampuni tanzu ya TPDC, Joseph Kavishe alisema bomba la Mtwara mpaka Dar es Salaam lina km 551 huku likiwa na uwezo wa kusafirisha gesi asilia za futi za ujazo milioni 784 kwa siku bila mgandamizo.

Alisema katika uzalishaji wa umeme kituo cha Kinyerezi 1 hutumia gesi asilia za ujazo wa milioni 30, Kinyerezi II milioni 33 na Ubungo milioni 33 hivyo kwa siku hutumia gesi za futi za ujazo milioni 90 kwa siku sawa na asilimia 11 ya uwezo wa bomba hilo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here