SHARE

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepongezwa kwa kununua boti ya ulinzi katika bandari ya Mtwara, ambayo itasaidia kufanya doria na kuimarisha usalama wa bahari hiyo.

Akizungumza wakati wa kuzindua boti hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa (pichani) alisema kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, itashirikiana na TPA ili kuhakikisha kuwa ukanda wa bahari na mkoa, unakuwa katika hali ya salama wakati wote.

“Mbali na watu kutumia bahari hiyo kusafi risha magendo lakini wapo watu wanaotumia nafasi zao kuharibu maboya ambayo yanasaidia meli kuingia na kutoka bandarini hali ambayo inaleta hofu zaidi,” alisema Byakanwa.

Alisema; “Ujio wa boti hii utaongeza usalama zaidi katika bahari ambapo tunaamini kuwa tutapata ushirikiano mzuri zaidi utakaojenga na kuimarisha usalama wa bandari na mkoa wetu.

“Biashara ya magendo hatutairuhusu iendelee kufanyika katika mkoa wetu, tutawadhibiti, haiwezekani TPA itoe zaidi ya Sh bilioni 4 kununua boti halafu sisi tusiitendee haki,” alisema Byakanwa.

Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Nelson Mlali alisema kuwa hivi sasa bandari hiyo, ina ongezeko la shehena zaidi ya tani 300,000, tofauti na mwaka 2005 ambapo shehena iliyokuwa ikihudumiwa ilikuwa ni tani 100,000.

Alisema, ongezeko hilo linahitaji uaminifu na usalama zaidi na kuwa ujio wa boti ya ulinzi utaimarisha ulinzi katika ukanda wa bahari na kuongeza usalama wa bidhaa zitakazosafirishwa kupitia bandari hiyo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here