SHARE

WAKATI alipotembelea nchini mwaka 1990, miongoni mwa ziara za awali kabisa za Mzee Nelson Mandela, baada ya kutoka kifungoni wakati huo hajawa Rais, alifika nchini Tanzania.

Hapana shaka ni eneo alilolipa hadhi ya ‘nyumbani’ kwani mbali na nafasi kubwa iliyokuwa nayo kama kiongozi wa kutetea ukombozi wa Afrika, pia Taifa na Watanzania, wana mengi katika kumuwezesha akakombolewa.

Mandela, baadaye alishangazwa alipokumbushwa kwamba alipopita miongo mitatu awali, alisahau viatu vyake nchini akiwa katika harakati zake za kukomboa Afrika Kusini, yenye ubaguzi wa rangi.

Ikumbukwe, ni miaka miwili tu baada ya ziara hiyo, alifungwa jela na alitoka kwa msamaha miezi kabla ya kuzuru tena nchini Tanzania.

Viatu hivyo aliviacha katika nyumba aliyofikia na pale alipokumbushwa akionyeshwa kiatu chake, Mzee Mandela alishangazwa sana kutunziwa kwa siku hizo zote. Aliangua kicheko kikubwa, pale alipokikumbuka, kukijirabu kukivaa na akabaini bado vinamtosha.

ILIVYOKUWA

Alifikia nyumba gani? Vicky Nsilo Swai (71) na familia yake, wana simulizi ndefu ambayo hadi Mzee Mandela anarudi tena nchini, ilishatimu miaka 33.

Vicky, ambaye katika miaka ya karibuni alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro.

“Nakumbuka wakati Hayati Nelson Mandela alipotembelea Tanzania mwaka 1962, wakati nikiishi na marehemu mume wangu Mzee Asanterabi Nsilo Swai,” Vicky, anasimulia ilivyokuwa na kuongeza;

“Wakati huo (mume) akiwa waziri katika serikali iliyokuwa ikiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar-es-Salaaam, alisahau viatu vyake nyumbani kwetu siku alipoondoka.”

Anasema Mzee Mandela alipoondoka kurejea nchini Afrika Kusini, alilazimika kuacha baadhi ya mizigo, ikiwemo viatu vyake, kutokana na kuwa na mizigo mingi.

Mama Vicky anasema, kutokana na maamuzi hayo yeye na mumewe, Mzee Nsilo Swai, walivihifadhi kwa muda huo wote na anaongeza:

“Mara baada ya mume wangu Mzee Swai kustaafu masuala ya Siasa, tulihama kutoka Dar-es-Salaam na kurudi hapa Moshi mkoani Kilimanjaro na vitatu vya Mandela.”

Anasema, marehemu mume wake, Mzee Nsilo Swai, baadaye alipata kazi katika Umoja wa Mataifa, jijini New York Marekani, ambako alienda na viatu aina ya mabuti vya Mzee Mandela. Huko waliishi kwa miaka 15.

“Tulivihifadhi viatu hivyo kwenye kabati lililokuwemo chumbani kwetu na sikuwahi kuvipaka rangi ya viatu, wala kuviosha zaidi ya kuweka vipande vya magazeti kukuuu, ili visipoteze muundo wake,” anaeleza Mama Vicky.

Anasema, katika hali iliyomshangaza hata yeye, ni kwamba viatu hivyo viliendelea kuonekana vipya kila siku, hata pale alipovirejesha nchini Afrika Kusini mwaka 1995, ikiwa ni baada ya miaka 33 za kuzihifadhi vilionekana bado vipya kabisa.

”Viatu hivyo bado vilimkaa Mandela ambaye nakumbuka wakati namkabidhi alitania viatu hivi vimetembea kuliko mimi mwenyewe,” anasimulia Mama Vicky, huku akitabasamu.

Mama huyo anasema tendo hilo liliwaletea wengi mshangao namna alivyovuitunza viatu hivyo kwa miaka 33, vikiwa katika hali ya upya wake.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here