SHARE

Rais mpya wa Botswana, Mokgweetsi Masisi amemtaka Rais Joseph Kabila kutojitokeza tena kuwania urais wakati wa uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambao umecheleweshwa sana akisema amekuwa madarakani kwa muda mrefu.

Botswana, moja ya nchi za Afrika zilizoimarika katika demokrasia, ndiyo nchi pekee ambayo imethubutu kumkosoa Kabila.

Mapema mwaka huu, serikali ilitoa taarifa rasmi ikimlaumu wazi rais wa DR Congo kwa kuwa kiini cha kuzorota kwa ubinadamu na ukosefu wa usalama.

“Rais wa DRC amekaa mamlakani muda mrefu kuliko muda aliotarajiwa,” Masisi ambaye aliingia madarakani mwezi huu alisema hayo katika mahojiano na Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo mjini London, Alhamisi iliyopita.

“Matumaini yetu tunaweza kupata msimamo wake kamili (Kabila) wa kutothubutu kurudi madarakani kwa namna yoyote iwayo.”

Wapinzani wa Kabila wanahisi kwamba anataka kupitisha kura ya maoni ili abadili Katiba ya DR Congo imruhusu kuwania urais kwa mihula zaidi ya miwili kama walivyofanya viongozi wa nchi jirani za Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Congo.

Kabila hajathibitisha wala kukanusha madai hayo lakini hatua yake ya kukataa kujiuzulu mwishoni mwa mwaka 2016 muhula wake ulipomalizika ilichochea maandamano mitaani. Alitumia vikosi vyenye silaha hali iliyoibua shaka kwamba nchi hiyo ingeweza kutumbukia kwenye machafuko.

Uchaguzi mkuu wa DR Congo, ikiwa hakutakuwa na mabadiliko, umepangwa kufanyika Desemba 23.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here