SHARE

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo kipo hatarini kuchukuliwa hatua kali na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya jana serikali kuitaka itoe muda wa mwezi mmoja kwa Chadema kuwasilisha taarifa za hesabu zake.

Taarifa hizo zinatakiwa baada ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini dosari kwenye taarifa za fedha za chama hicho.

Mbali na Chadema, vyama vingine ambavyo viko katika hatari hiyo ni ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Magaeuzi na CCM, ambavyo vimetakiwa kuwasilisha kwa Msajili taarifa za fedha zake na chama kitakachobainika kuwa na upungufu na kile kisichowasilisha taarifa hizo kwa mujibu wa sheria, kichukuliwe hatua kali.

Adhabu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwa chama kitashindwa kuwasilisha kwa Msajili taarifa zake za hesabu zilizokaguliwa na CAG au kuwa na upungufu ni pamoja na kusitishiwa ruzuku na kushtakiwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari na Elimu Bunge mjini hapa jana, alisema ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17, imeonyesha Chadema inaoongoza kwa upungufu ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa malipo yasiyo na nyaraka au nyaraka zenye upungufu.

Waziri huyo alikuwa anazungumzia hoja zilizoibuliwa na CAG Prof. Mussa Juma Assad na kuelekezwa kwa wizara yake katika ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni Aprili 14.

Kabla ya kutoa maagizo ‘mazito’ kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, waziri huyo alisema kuwa kwenye ripoti ya CAG imebainika vyama vya siasa tisa kati ya 19 havijawasilisha ripoti zake za hesabu kwa CAG ili kukaguliwa.

“Katika mwaka ulioishia Juni mwaka jana, ripoti ya CAG inaonyesha ni vyama 10 tu kati ya 19 vilivyosajiliwa ndiyo vimewasilisha taarifa zao za hesabu kwa CAG, baadhi ya vyama hivyo ni CCM, SAU, Chadema, NLD, DP, CCJ, ADC, AFP na Demokrasia Makini,” alisema Mhagama.

Aliongeza kuwa kati ya vyama hivyo, vitatu ambavyo ni CCM, Chadema na NLD ndiyo vinavyopata ruzuku.

Alivitaja vyama tisa ambavyo havijawasilisha taarifa zake za hesabu kwa CAG kuwa ni pamoja na CUF, UPDP, NCCR-Mageuzi, NARA, ACT-Wazalendo na UMD. Kati yake, CUF, NCCR na UDP vinapata ruzuku ya serikali.

“Ripoti hii ya CAG inaonyesha kuwa vyama hivi vya siasa vinazidi kutoiheshimu Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo miaka ya nyuma ni vyama vinne tu ndiyo havikuwasilisha taaifa zake za hesabu kwa CAG lakini mwaka huu vimepanda na kufikia tisa,” alisema waziri huyo na kueleza ziadi:

“Katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa CAG, namwagiza Msajili avitake vyama vyote vilivyosajiliwa kuwasilisha hesabu zao ndani ya mwezi mmoja na pale atakapobaini kuwapo kwa upungufu wa kisheria achukue hatua za kisheria kwa chama chochote kile kitakachobainika.”

Akifafanua zaidi kuhusu upungufu uliobainishwa na CAG kwa vyama vilivyowasilisha taarifa ya hesabu zake, Mhagama alisema baadhi ya vyama vikiwamo SAU, CCJ na AFP hesabu zake zilikuwa chini ya viwango, muundo wa hesabu haukuwa sawa na hesabu kutofautiana.

Mhagama pia alisema baadhi ya vyama vikwiamo Chadema, NLD na Demokrasia Makini viliwasilisha hesabu zao bila kuwa na rejista za mali zao za kudumu jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya vyama vya siasa.

Alisema pia baadhi ya vyama hivyo havikuwa na usuluhishi wa fedha wa kibenki jambo ambalo ni takwa la kisheria.

MKOPO WA MWAKA

Aliongeza kuwa baadhi ya vyama vikiwamo Chadema, SAU na ADC vilikuwa na upungufu katika malipo yenye nyaraka ya zaidi ya Sh. milioni 735.9.

“Katika ripoti hii, Chadema iliongoza kwa kuwa na malipo yasiyo na nyaraka au kuwa na nyaraka zenye upungufu. Pia ilikuwa na masurufu yasiyorejeshwa yenye thamani ya kiasi cha Sh. milioni 400,” alissema.

Waziri huyo aliendelea kueleza kuwa ripoti hiyo ya CAG ilibainisha Chadema kilikuwa na mkopo wa mwaka 2014/15 wa Sh. milioni 158.8 uliorejeshwa bila nyaraka iliyothibitisha uhalali wa malipo pamoja na mkopo mwingine wa Sh. bilioni mbili uliorejeshwa bila nyaraka hizo muhimu.

Aliongeza kuwa chama hicho kilionekana hesabu zake zina malipo ya ‘tax invoice’ yenye thamani ya Sh. milioni 866.6 zilizolipwa kwa ajili ya mabango na Sh. milioni 715 zililipwa kwa mwanachama kama fedha iliyokopwa kwa ununuzi wa mabango bila nyaraka.

“Kulikuwa pia na makusanyo ya Sh. bilioni 2.3 yaliyolipwa kinyume cha sheria ya chama hicho cha Chadema. Yapo manunuzi ya Sh. bilioni 2.1 yaliyofanyika bila ushindani,” alisema.

Kwa upande wa CCM, Mhagama alisema ripoti ya CAG imebainisha uwapo wa Sh. milioni 33.1 zilizohamishwa kutoka kwenye akaunti ya pensheni kwenda kwa Katibu Mkuu pamoja na uwapo wa mikopo iliyowekezwa kwenye kampuni kadhaa zikiwamo Uhuru na TOT ambayo haionyeshi faida.

“Napenda kumshukuru CAG kwa kutukumbusha kuwa kwa mujibu wa sheria serikali inapaswa kusimamia uwajibikaji wa vyama hivi vya siasa,” alisema Mhagama.

Alitaja hatua ambazo Msajili wa Vyama vya Siasa anaweza kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria endapo chama kitabainika kwenda kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa, ni pamoja na kusitisha ruzuku ya serikali kwa chama kilichokiuka kuwasilisha maelezo ya matumizi ya fedha hiyo na chama hicho kuondolewa kwenye ruzuku kama kiasi cha fedha kilichotumika hakina maelezo.

“Lakini pia kama mali au hesabu za chama zinaonekana kuwa na picha ya kijinai, msajili anaweza kukipeleka chama husika polisi,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here