SHARE

Waziri Mkuu, Dk Abiy Ahmed ametangaza kusudio lake la kuifanyia marekebisho katiba ili iingizwe ibara inayozungumzia ukomo wa uongozi kwa ofisi hiyo kuwa vipindi viwili.

Dk Ahmed aliwaambia maelfu ya watu waliompokea katika mji mkuu wa jimbo la Kusini, Hawassa, akisema amedhamiria kuhakikisha anaimarisha misingi ya demokrasia katika mageuzi anayofanya.

Safari katika mji huo ni sehemu ya ziara anazofanya nchi nzima tangu alipochaguliwa kuwa waziri mkuu, Aprili 2.

“Kiongozi yeyote katika nchi hii hataruhusiwa kutumikia ofisi hii kupindukia vipindi viwili baada ya kufanya marekebisho katika katiba,” alisema Abiy.

Katiba ya sasa inasema kwamba muhula wa uongozi kwa waziri mkuu hauna ukomo.

Ethiopia inatumia mfumo wa kibunge ambapo chama kinachokuwa na wabunge wengi ndani ya bunge ndicho kinamteua waziri mkuu.

Abiy alimpongeza mtangulizi wake, Hailemariam Desalegn, kwa kukataa vishawishi vya kumtaka ang’ang’anie madaraka.
Desalegn alijiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu na mwenyekiti wa muungano unaotawala wa EPRDF Februari mwaka huu.

“Hailemariam alijiuzulu wakati ambao alikuwa na uwezo wa kuendelea kuchangia pa kubwa nchini, hata hivyo, kuna viongozi ambao huwa wanakataa kung’atuka madarakani ingawa wanatakiwa kustaafu,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here