SHARE

Watu wengine wanajiwekea malengo ya kuvunja rekodi katika kazi, biashara, ujasiriamali au hata michezo. Lakini wapo wanaoweka malengo ya kipekee.

Jessica Nabongo ni mmoja wao. Mfanyakazi huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) aliacha kazi kutimiza ndoto yake ya kuizunguka dunia.

Ingawa alikuwa na mshahara mzuri na nyumba nchini Marekani, vyote hivyo havikukamilisha ndoto yake ambayo ni kuweka rekodi ya kutembelea kila nchi duniani.

Katika safari yake ya kuzunguka dunia alianza kama utani kujikuta akisafiri kutoka bara moja kwenda jingine jambo ambalo anasema huenda lilichochea hamu ya kutaka kuizunguka dunia.

Alianza kufundisha lugha ya Kiingereza nchini Japan, halafu akaenda Uingereza kusomea sheria kisha akarudi Marekani na kuajiriwa katika UN na kuhamishiwa nchini Benin kisha Italia.

Mwanamke huyo mwenye asili ya Uganda alianza kupenda kusafiri na mara moja akaamua kuacha kazi, kupangisha nyumba yake na kuhamia nchini Japan.

Kwa kuwa alihofu angepata usumbufu wa kutafuta saluni awapo safarini, alikata nywele na kubaki na upara ambao sasa umekuwa utambulisho wake.

Kwa nini ameamua kuzunguka dunia?

Mwanamke huyo anasema lengo lake ni kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuzunguka dunia kwa kuwa rekodi hiyo inashikiliwa na watu weupe.

Mpaka sasa kuna rekodi ya watu 150 waliozunguka nchi zote duniani na kati yao hakuna anayetumia pasipoti ya kutoka popote Afrika.

Mbali na hilo, anasema anafurahi kuishi kama wenyeji wake hivyo anapofika katika nchi lazima ajifunze tamaduni na kujichanganya.

Tangu alipoanza safari yake hiyo mwaka juzi, Jessica amekwishatembelea nchi 109 na Tanzania ikiwamo. Lengo lake ni kutembelea nchi 172 mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Anajua atakabiliwa na kibarua kigumu kutembelea nchi za Korea Kaskazini na Iran kwa kutumia pasipoti ya Marekani, hivyo amejipanga kuitumia ya Uganda.

Anapata wapi fedha?

Pamoja na kuwa anamiliki nyumba nchini Marekani ambayo ameipangisha, Jessica ameungana na vijana wa Kiafrika Jet Black ambao huunganisha watu maarufu na hoteli kwa ajili ya biashara ya mali kwa mali.

Kwamba si kila hoteli au ndege anayotumia hulipia, vingine huwa ni udhamini ambao unawezeshwa na vijana hawa kwa makubaliano kuwa atawatangaza katika kurasa zake za mitandao ya kijamii. Pia huchangisha fedha katika mtandao maarufu wa GoFundMe.

Changamoto anazokutana nazo

Kuwa mwanamke anayesafiri peke yake kumemfanya apate changamoto kila mara hasa ya kuonekana kahaba anayejiuza kimataifa.

“Mara kadhaa wanaume hunitongoza wakiamini nimefika mahali hapo kwa ajili ya biashara ya mwili, madereva wa taksi, wahudumu hunichukulia hivyo,” anasema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here