SHARE

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza nyongeza ya asilimia tano kwa kiwango cha chini cha mshahara nchini Kenya.Huku akisisitiza uwepo wa mazungumzo kutatua migogoro ya migomo.

Nyongeza hiyo ya mishahara imetangazwa na Waziri wa Kazi Balozi Ukur Yatani Kanacho aliyemwakilisha Rais Kenyatta wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani.

Maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kwenye viwanja Uhuru Park pia yamehudhuriwa na viongozi wengine mashuhuri kutoka serikalini.

Mwaka 2017 Rais Kenyatta alihudhuria na kuhutubia taifa lakini mwaka huu 2018 mambo yamekuwa tofauti ambapo Waziri Yatani ndiye amemwakilisha kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa hotuba ya Rais iliyosomwa na waziri huyo, Serikali imetangaza kuwaongezea watumishi wa umma nyongeza ya asilimia tano ya mshahara.

Hotuba hiyo imelenga mambo manne yakiwamo kuangazia usalama wa chakula nchini, makazi bora na nafuu, ujenzi wa viwanda ili kukabiliana na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, na matibabu bora.

Kenyatta mwaka 2017 alitangaza nyongeza ya asilimia 18 kwa wafanyakazi wa umma.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli amesema agizo hilo halijatekelezwa kwa baadhi ya kampuni na taasisi.

“Kuna kampuni nyingi hazijatekeleza agizo hilo. Rais pia alipendekeza ushuru kwa wanaopokea mshahara wa chini ya Sh100,000 upunguzwe lakini hayo yote hayajazingatiwa,” amesema Atwoli.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyehudhuria maadhimisho hayo, amesema mkataba wa salamu zake na Rais Uhuru Kenyatta wa Machi 2018, ulilenga kuimarisha maisha ya Wakenya.

“Mazungumzo yetu yaliegemea kuimarisha maisha ya wananchi wote, kwa msingi wa bidhaa na kodi nafuu ya nyumba,” amesema Odinga.

Ameongeza kuwa Nasa imeungana na Serikali ya Jubilee ili kuangazia matatizo yanayowakumba Wakenya ikiwamo kukabiliana na kero za ufisadi.

Wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni; Waziri wa Elimu Amina Mohamed, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Peter Kimunya, Musalia Mudavadi, Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Nairobi Esther Passaris, mbunge maalum wa ODM na katibu wa KNUT Wilson Sossion na viongozi wengine mashuhuri serikalini.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here