SHARE

CHAMA cha Wananchi (CUF), upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kimewataja Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi na Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili, Prof. Ibrahim Lipumba, kuwa kikwazo hesabu za chama kukaguliwa.

Hesabu za chama hicho zilitakiwa kisheria kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Taarifa iliyotolewa jana na Maalim Seif ilieleza hayo na kufafanua kuwa kukosekana kwa taarifa ya fedha ya chama si tatizo la chama chenyewe, hali hiyo ilisababishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa na Prof. Lipumba dhidi ya chama hicho.

“Kupitia taarifa hii, CUF inapenda kuutarifu umma kuwa kukosekana kwa taarifa ya fedha ya chama si tatizo la chama chenyewe bali msajili wa vyama vya siasa na Prof. Lipumba,” ilieleza taarifa hiyo.

Wakati akiwasilisha bungeni ripoti yake ya mwaka 2016/17, CAG Prof. Mussa Assad alibainisha kuwa kati ya vyama 19 vilivyosajiliwa usajili wa kudumu, vyama tisa havikuwasilisha taarifa za fedha za kila mwaka.

CAG Prof. Assad alisema kuna ongezeko la vyama kutoka vyama vinne mpaka tisa ambavyo havikuwasilisha hesabu zao.

Kwenye taarifa ya CUF, Maalim Seif alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa mwaka 2010/11, CUF hakijawahi kushindwa kuwasilisha hesabu zake kwa ajili ya ukaguzi.

Alieleza kuwa mapungufu yaliyoainishwa katika taarifa ya CAG ya kutokuwa na rejista ya mali za chama, kutofanyika kwa usuluhishi wa kibenki yalizungumzwa katika vikao vya chama na kuwekewa utaratibu wa kufanyiwa kazi.

Alisema, kwa kuwa mwaka wa fedha wa chama ulikuwa unaanzia Januari hadi Desemba na kupishana na mwaka wa serikali wa Julai hadi Juni, makubaliano yalifikiwa na ofisi ya CAG kubadilisha mwaka wa fedha wa chama.

“Makubaliano hayo yaliafikiwa na vikao vya Bodi ya Wadhamini na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na hivyo ukaguzi wa nusu mwaka wa 2014/2015 ulifanywa na CAG na ilibakia kikao cha chama ambacho kilipangwa kufanyika Septemba 26, 2016, ofisi kuu ya chama Buguruni Dar es Salaam,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema kikao hicho hakikufanyika kutokana na ofisi kuu kuvamiwa na Prof. Lipumba Septemba 24, 2016.

Alisema taarifa ya uvamizi huo ilipelekwa kwa CAG kupitia barua Kumb.Na.CUF/AKM/003/016/051ya Oktoba 14, 2016. Iliyokuwa inataarifu juu ya kushindikana kufanyika kikao cha chama na uwasilishaji taarifa ya hesabu za chama zilizofungwa za mwaka 2015/2016.

Kwa mujibu wa Maalim Seif, tangu wakati huo, Jaji Mutungi na Prof. Lipumba wameingilia fedha na mali za CUF na jukumu la kuandaa taarifa ya hesabu za chama na kuikabidhi kwa CAG kwa ajili ya ukaguzi halikuwa kipaumbele kwao.

Alisema kutokana na msajili kutomtambua yeye kama katibu na badala yake kuanzisha cheo kipya kisichokuwa cha kikatiba cha kaimu katibu mkuu na kumteua Magdalena Sakaya kwa nafasi hiyo, kumeathiri mawasiliano na ofisi ya CAG.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here