SHARE

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema yuko tayari kujiunga na Rais Uhuru Kenyatta katika juhudi za kuunganisha Wakenya na kuzika siasa za mgawanyiko.

Musyoka amepongeza hatua ya Rais Kenyatta kuanza mikakati ya kuunganisha Wakenya kwa ushirikiano na kiongozi wa upinzani Raila Odinga Machi 9, 2018.

Musyoka pia amempongeza rais kwa kuomba msamaha kwa kutoa matamshi ya kugawanya Wakenya wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2017.

Makamu huyo wa rais wa zamani, amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli moja eneo la Elementaita, Nakuru wakati wa kufunga kongamano la siku mbili la viongozi wa Wiper.

“Ningependa kumpongeza Rais Kenyatta kwa kujitokeza wazi na kuomba Wakenya msamaha. Ni viongozi wachache mno wanaoweza kunyenyekea na kuomba wananchi msamaha.

Nimempa hongera kwa hilo. Huu ni wakati wa kusamehe na kuhubiri amani,” amesema Musyoka.

Musyoka amesema anapanga kukutana na Rais Mstaafu Daniel Arap Moi hivi karibuni.

“Ninapanga pia kumtembelea Rais Mstaafu Mwai Kibaki na mama yake Rais, Mama Ngina Kenyatta,” amesema Musyoka.

Musyoka amemkejeli Naibu wa Rais William Ruto ambaye juhudi zake za kukutana na Mzee Moi ziligonga mwamba wiki iliyopita.

“Walioshindwa kumwona Rais Mstaafu Moi wajaribu tena,” amesema Musyoka.

Amesema mwafaka baina ya Rais Kenyatta na Odinga unastahili kuleta maendeleo mbali na kusuluhisha mizozo ya kisiasa.

Nasa kusajiliwa

Amesisitiza kuwa muungano wa Nasa bado ni thabiti huku akisema kuwa atashinikiza Nasa isajiliwe kama chama cha kisiasa.

Amesema Odinga hajajiunga na Chama cha Jubilee na bado yuko katika upinzani.

Amesema kabla ya Rais Kenyatta na Odinga kusalimiana, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kushinikiza viongozi hao wawili wakutane ili kuzungumza.

“Nilikuwa katika mstari wa mbele kuwataka Rais Kenyatta na Odinga wakutane na kusitisha siasa za mgawanyiko. Inaonekana Odinga alisikia wito wangu na akakubali kukutana na Rais Kenyatta japo hakunifahamisha,” akasema Musyoka.

“Chama cha Wiper kiko tayari kuanzisha mchakato wa kuunganisha nchi na kuhubiri amani,” aliongeza.

Musyoka pia amesema anaunga mkono Katiba kufanyiwa mabadiliko.

“Niliitwa tikitimaji kwa sababu nilisema kuwa Katiba ilifaa kuangaliwa kwa umakini. Sasa Wakenya wameona umuhimu wa niliyosema. Chama cha Wiper kinaunga mkono mabadiliko ya Katiba na tunafaa kujadili suala hili kwa umakini,” amesema Musyoka


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here