SHARE

WAKATI wakiwa wamekaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, mshambuliaji tegemeo wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema wao wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi zote tatu zilizobaki katika ligi hiyo inayoshirikisha klabu 16.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, imebakiza mechi tatu dhidi ya Singida United ambayo itapigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida, halafu itarejea Dar es Salaam kuikaribisha Kagera Sugar na kisha itasafiri kuifuata Majimaji ya Songea katika siku ya mwisho ya funga dimba Mei 28, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti la Nipashe jana, Okwi alisema akili na mawazo ya wachezaji wa timu hiyo ni kupambana kupata matokeo mazuri katika mechi hizo na si kusaka pointi mbili ambazo zinazungumzwa kwa kuangalia hesabu za haraka haraka.

Okwi, ambaye yupo kileleni mwa orodha ya wafungaji bora msimu huu akiwa na mabao 20 katika ligi hiyo, alisema wanafahamu msimu wa ligi una mechi 30 na wao mpaka juzi wamecheza michezo 27, hivyo hawajamaliza kazi yao kwa msimu huu.

“Bado hatujamaliza kazi, tumebakiza mechi tatu na zote tunahitaji kupata matokeo mazuri, mapambano bado yanaendelea, hatusemi kuwa tumebakiza pointi moja,” alisema mshambuliaji huyo raia wa Uganda ambaye aliwahi pia kuichezea Yanga.

Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 65, huku ikifuatwa na Azam FC yenye pointi 49 ambayo haiwezi kufikisha pointi hizo hata ikishinda michezo yake iliyobakia, wakati Yanga yenye pointi 48 ina uwezo wa kufikisha pointi 66 endapo itashinda mechi zake sita zilizosalia.

Vinara hao walisafisha njia ya kuelekea kutwaa ubingwa huo rasmi baada ya kuwafunga watani zao bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Aprili 29, mwaka huu na juzi ilipopata ushindi wa idadi hiyo ilipowakaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara.

Bingwa wa ligi hiyo atapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Singida United ambayo imetinga fainali ya Kombe la FA ina nafasi kubwa ya kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here